Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 09, 2024 Local time: 03:02

Kura zahesabiwa Burkina Faso, upinzani wadai kufanyika udanganyifu


Zoezi la kuhesabu kura linaendelea nchini Burkina faso baada ya uchaguzi mkuu ambao uligubikwa na mashambulizi ya makundi ya waasi nchini humo.

Wagombea wa vyama vya upinzani wamedai kuwepo wizi wa kura wakati wa uchaguzi.

Rais Roch Marc Christian Kabore anatarajiwa kushinda muhula mwingine madarakani, wafuasi wake wakiwa na Imani kwamba atapata ushindi wa moja kwa moja.

Rais Roch Marc Christian Kabore amekuwa akihimiza wapiga kura wote wa Burkina faso kushiriki katika uchaguzi huo.

"kwa hivyo, nawahimiza wa Burkinafaso kutozembea na kushiriki katika upigaji kura kwa sababu hii inahusu demokrasia nchini Burkinafaso, inahusu maendeleo ya Burkinafaso na inahusu sana usalama wan chi yetu.”

Lakini uchaguzi kumchagua rais na wabunge haujafanyika katika maeneo ambayo makundi ya wanamgambo yamekuwa yakitekeleza mashambulizi karibu kila siku.

Mapigano hayo yamepelekea zaidi ya watu milioni moja kutoroka makwao katika muda wa miaka miwili iliyopita.

Watu 1,200 wameuawa tangu mwaka 2015.

Mashambulizi kutoka kwa makundi ya wapiganaji

Ukosefu wa usalama limekuwa swala kuu katika kampeni na wanajeshi wameshika doria katika sehemu mbalimbali za nchi wakati wa kampeni na uchaguzi katika nchi hiyo ya Afrika magharibi ambayo ni miongoni mwa nchi maskini sana Afrika.

Wagombea 12 wa upinzani wanaowania urais dhidi yar ais Kabore, wamemkosoa kwa kushindwa kukomesha umwagikaji wa damu.

Kiongozi wa upinzani ambaye alimaliza katika nafasi ya pili katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 Zephirin Diabre, amegombea urais kwa mara nyingine tena kupitia chama cha aliyekuwa rais Blaise Compaore.

Amedai kuwepo mipango ya kufanyika udanganyifu katika uchaguzi huo na kutaka wafuasi wake kuwa waangalifu sana wakati wa kuhesabu kura.

"Wapiga kura wote wa Burkina faso wanakubaliwa kuingia katika vituo vya kupigia kura na kushuhudia zoezi la kuhesabu kura. Hivyo ndivyo sheria inavyosema. Kwa hivyo, nahimiza kila mmoja wenu kufanya hivyo ili kuhakikisha kwamba hakuna udanganyifu unafanyika.”

Mazungumzo na makundi ya wapiganaji

Compaore, ambaye alipinduliwa kufuatia maandamano ya mwaka 2014 baada ya kuwa madarakani kwa miaka 27, yupo mafichoni lakini baadhi ya wapiga kura wanataka utawala wake.

Kampeni zilifanyika huku mashambulizi ya makundi ya wanamgambo yakiendelea na kusababisha umwagikaji wa damu.

Hakuna visa vya mashambulizi vimeripotiwa jumapili wakati upigaji kura unaendelea.

Karibu washindani wote wa Kabore wametaka kufanyike mazungumzo kati ya serikali na makundi ya wapiganaji, lakini Kabore amelikataa pendekezo hilo.

Karibu watu milioni 6.5 wamesajiliwa kupiga kura Burkinafaso, lakini upigaji kura haukufanyika katika karibu vijiji 1,500 kutokana na ukosefu wa usalama.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG