Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Oktoba 04, 2024 Local time: 17:05

Kundi la kwanza la wakimbizi wa Burundi laondoka Tanzania


Wakimbizi wa Burundi
Wakimbizi wa Burundi

Wakimbizi takriban 600 wameondoka Tanzania na kurudi majumbani kwao katika nchi jirani ya Burundi Alhamisi.

Umoja wa mataifa umeeleza kuwa hili ni kundi la kwanza katika kundi la wakimbizi wengi wanaotarajiwa kurudishwa makwao huku baadhi ya wahamiaji wakiwa na wasi wasi watarudishwa bila ridhaa yao.

Kundi hilo la kwanza lililorejeshwa nchini Burundi ni kutoka kambi ya Nduta, Nyarugusu na Mtendeli katika mkoa wa Kigomba. Kulingana na wizara ya mambo ya ndani ya Tanzania, wakimbizi hao walikubali kujiorodhesha na kurudi kwao kwa hiari yao. Igwe Athumani, ni muakilishi wa wizara ya mambo ya ndani mkoani Kigoma, anasema wameanzisha zoezi hilo sababu hali ya usalama ni shuari nchini Burundi.

Lakini bado kuna wakimbizi ambao hawako tayari kurejea nchini mwao, wakidai kwamba usalama haujakamilika. Wakimbizi hao wanahofu kwamba watarejeshwa nyumbani kwa nguvu, kutokana na baadhi ya hatua ngumu ambazo zilichukuliwa kambini, amesema Miburo Elie, mkimbizi kutoka kambi ya Nyarugusu.

Igwe Athumani anasema hoja za wakimbizi hao hazina msingi, anasema serekali ya Tanzania itaendelea kuwahamasisha kurudi Burundi kuendelea na shughuli za kilimo na kazi nyingine.

Takriban wakimbizi laki mbili walikimbilia katika nchi jirani ya Tanzania. Shirika la umoja wa mataifa linalohudumia wakimbizi, UNHCR limesema katika zoezi hili ambalo linafanyika, halijahusika kuwahamasisha wakimbizi kurudi nyumbani.

UNHCR inaendelea kuomba serekali za Burundi na Tanzania kuheshimisha mikataba ya kimataifa , ili kuhakikisha kwamba hakuna mkimbizi anarejeshwa nyumbani bila ridha yake.

Maelfu ya raia wa Burundi walikimbia ghasia za kisiasa zilizoongezeka wakati Rais Pierre Nkurunziza alipoamua kugombea muhula wa tatu na wapinzani wake kumlaumu kuwa amevunja katiba ya nchi.

Tume ya Umoja wa Mataifa juu ya Burundi iliripoti mwezi Septemba kwamba kuna hatari ya ghasia nyingine kuibuka wakati nchi hiyo ikijiandaa kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 huku mzozo wake wa kisisasa ukiwa bado haujasuluhishwa.

Lakini Burundi na Tanzania waliweka makubaliano mwezi Agosti kuanza kuwarudisha wakimbizi laki mbili wa Burundi wakisema kwamba hali katika nchi hiyo imeboreka zaidi.

Wakati huo huo afisa mmoja wa serikali ya Tanzania na Umoja wa mataifa wamesema wakimbizi wote walioondoka leo wanarudi nyumbani kwa hiari yao.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Patrick Nduwimana, Washington, DC.

XS
SM
MD
LG