Rais wa Ecuador amesema kwamba kujenga upya baada ya tetemeko la ardhi lenye nguvu lililotokea nchini humo siku ya Jumamosi kutagharimu mabilioni ya dola.
Rais Rafael Correa, aliutembelea mji wa kaskazini mashariki wa Portovieji Jumatatu ili kujionea mwenyewe athari za tetemeko hilo la ardhi lililokuwa na nguvu ya 7.8 kwa kipimo cha rikta. Mji huo pamoja na miji mingine iliyo karibu ya Manta na Pedernales, ndiyo iliyoathirika sana, ingawa uharibifu ulienea kote nchini humo.
Serikali imesema kwamba itakopa dola milioni mia sita kutoka kwa mashirika ya kimataifa, pamoja na benki ya dunia, ili kufadhili juhudi zake za majibu ya dharura. Uchumi wa taifa hilo dogo la Marekani ya Kusini ambalo ni mwanachama wa OPEC umedorora kutokana na kushuka kwa bei ya mafuta.