KCNA, shirika la habari la serikali ya Korea Kaskazini limeripoti Jumamosi kwamba maendeleo haya ya karibuni ni matokeo ya ziara ya hivi karibuni ya afisa mwandamizi wa Umoja wa Mataifa katika taifa hilo lililotengwa.
Jeffrey Feltman, Naibu Waziri kwa masuala ya kisiasa katika Umoja wa Mataifa alitembelea Korea Kaskazini wiki hii na kufanya mikutano na Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kaskazini Ri Yoing Ho na naibu waziri wake wa mambo ya nje Pak Myong Guk.
Mwanadiplomasia huyo amekiri kuwa vikwazo vya kiuchumi vimeleta athari mbaya kwa msaada wa kibinadamu unaohitajika Korea Kaskazini.
Vyombo vya habari vya serikali ya Korea kaskazini vimeripoti kuwa ziara ya Feltman ilichangia kufahamiana kwa undani zaidi kati ya sekretarieti ya Democratic People’s Republic of Korea- DPRK na Umoja wa Mataifa.
Ziara ya Feltman imekuja mara tu baada ya Marekani na Korea kusini kufanya mazoezi ya anga makubwa zaidi ya pamoja mwaka huu. Mazoezi haya hufanyika kila mwaka.