Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Novemba 30, 2022 Local time: 16:58

Kobe Bryant na binti yake wafariki katika ajali ya helikopta


Mchezaji maarufu wa mpira wa vikapu Kobe Bryant ameaga dunia kufuatia ajali ya helikopta karibu na mji mdogo wa Calabasas katika jimbo la California.

Dunia yamkumbuka Kobe Bryant
please wait

No media source currently available

0:00 0:04:16 0:00

Bryant ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 41. Maafisa wa Los Angeles wamethibitisha kuwa miongoni mwa waliofariki katika ajali hiyo ni binti yake Kobe, Gianna, aliyekuwa na umri wa miaka 13. Jumla ya watu tisa walikuwemo katika helikopta hiyo na hakuna aliyenusurika.

Kulingana na vyombo vya habari Marekani ndege hiyo iliwaka moto kabla ya kuanguka, saa nne asubuhi saa za Marekani.

Ripoti zinasema kwamba kulikuwa na ukungu mzito katika sehemu ajali ilitokea, karibu na milima ya Calabasas.

Bryant alipata umaarufu sana kwa miongo miwili, akichezea timu ya Los Angeles Lakers, aliyoisaidia kushinda ligi ya basketball mara tano na kucheza michezo mikubwa sana 18 kabla ya kustaafu baada ya msimu wa mwaka 2016.

Kifo chake kinajiri saa chache baada ya kumtumia ujumbe wa twitter mchezaji maarufu wa basketiboli anayechezea Lakers, Le Bron James, akimsifia kwa kuvunja rekodi ya ufungaji na kumwondoa Kobe Bryant katika nafasi ya tatu ya wafungaji bora.

Bryant, aliyejulikana kama ‘black mamba’ alitarajiwa kutangazwa kuwa miongoni mwa wachezaji mashuhuri sana wa mchezo wa basketiboli katika kumbukumbu ya Naismith, mwezi ujao, tuzo ya juu kabisa kwa wachezaji nchini marekani.

Kutwa nzima Jumapili wachezaji wa sasa na wa zamani wa basketball nchini Marekani kuanzia Kareem AbdulJabbar, Michael Jordan, LeBron James na Shaquel O'neal ambaye alikuwa timu moja na Kobe, pamoja na makocha wa mchezo huo wamekuwa wakitoa rambi rambi.

Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama na Rais wa sasa Donald Trump pia walikuwa miongoni mwa watu waliotoa rambi rambi zao Jumapili.

Nyota huyo mara 18 wa mchezo wa basketiboli, anatambuliwa sana kama mmoja wa wachezaji wazuri sana wa mchezo huo duniani.

Alichaguliwa mwaka 2008 kama mchezaji wa bora wa msimu na baadaye kushinda dhahabu mbili, akichezea timu ya Marekani katika michezo ya Olimpiki.

Alishinda tuzo baada ya kutengeneza filamu fupi iliyopewa jina “dear basketball”, iliyoangazia shairi alilotunga kabla ya kustaafu mwaka 2016.

Ameacha mke – Venessa na watoto wasichana watatu Natalia, Bianca na Capri.

-Imetayarishwa na mwandishi wetu Kennes Bwire Washington DC

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG