Mshindi wa pili katika uchaguzi wa urais nchini Guinea Bissau amesema hatashiriki katika duru ya pili ya uchaguzi kwa madai kuwa utaratibu wa uchaguzi ulikuwa na wizi.
Kiongozi wa upinzani Kumba Yala alitoa maelezo hayo kwa waandishi wa habari alhamisi. Waziri mkuu wa zamani Carlos Gomes junior alishinda uchaguzi wa jumapili kwa asilimia 49 ya kura lakini sheria ya uchaguzi inataka kura zirudiwe kama hakuna mgombea yeyote atakayepata wingi wa kura unaohitajika. Yala ni mmoja wa wagombea watano ambaye anataka duru ya kwanza ya uchaguzi ibatilishwe kwa tuhuma za kutofuata taratibu za upigaji kura. Wafuatiliaji wa kimataifa wa uchaguzi walisema uchaguzi wa jumapili unaonekana ulikuwa huru na wa haki. Madai hayo ya wizi yameleta wasi wasi kuwa matatizo yako njiani katika taifa hilo ambalo limekuwa likikumbwa na mapinduzi, ambapo mkuu wa zamani wa upelelezi wa kijeshi, Samba Diallo aliuwawa saa kadhaa baada ya vituo vya uchaguzi kufungwa.
Kiongozi wa upinzani Guinea akataa duru ya pili ya uchaguzi.

Kiongozi wa upinzani akataa duru ya pili ya uchaguzi kwa madai ya wizi wa kura.