Mahakama maalum nchini Benin siku ya Jumanne ilimhukumu mmoja wa vigogo wa upinzani nchini humo, Joel Aivo, kifungo cha miaka 10 jela baada ya kesi ya uhaini ambayo wakosoaji wanasema ni utapeli wa kisiasa.
Viongozi kadhaa wa upinzani walikamatwa kabla au baada tu ya uchaguzi wa Aprili ambao ulishuhudia Rais Patrice Talon akishinda muhula wa pili kwa zaidi ya asilimia 86 ya kura.
Aivo, ambaye ni msomi aliwekwa kizuizini kwa miezi minane, alikana mashtaka ya kupanga njama dhidi ya serikali na biashara haramu ya mzunguko wa fedha.
Wakati uamuzi huo ulipotolewa mwendo wa saa tisa alfajiri siku ya Jumanne baada ya kusikilizwa kwa kesi iliyodumu kwa saa 16, wafuasi wachache wa Aivo waliokuwa bado mahakamani, wakiwa wamevalia fulana zilizosomeka, Profesa Aivo, watu wa Benin wako pamoja nawe.
Ilikuwa ni kesi ya udanganyifu ili kumtenga na siasa, Sosthene Armel Gbetchehou, mwanafunzi wa zamani wa mpinzani huyo aliyehukumiwa aliiambia AFP.
Aivo alikuwa miongoni mwa viongozi wa upinzani ambao walikuwa wamezuiwa kuwania katika uchaguzi wa urais nchini humo.