Kikosi kikubwa kabisa cha mapigano cha Marekani kimeondoka Iraq wiki mbili kabla ya tarehe iliyowekwa na rais Barack Obama kuondowa majeshi ya Marekani nchini humo.
Maafisa wa Pentagon wamesisitiza kwamba kiasi ya wanajeshi elfu 50 wa Marekani wanabaki Iraq kama kikosi cha mpito kutoa ushauri na mafunzo kwa jeshi la Iraq baada ya Ogusti 31.
Mashirika ya habari na vituo vya televisheni, baadhi vikiwa na waandishi habari walofuatana na wanajeshi walokua wanaondoka, walithibitisha kuondolewa kikosi cha pili cha jeshi la nchi kavu, kilichovuka mpaka na kuingia Kuwait kupitia kituo cha mpakani cha Khabari.
Hapajakuwepo na taarifa rasmi kutoka kwa rais Obama alipokua anarudi kutoka ziara yake ya majimbo matano kueleza mafanikio ya sera yake ya uchumi. Hata hivyo, katika wiki za hivi karibuni rais Obama, makamu rais Joe Biden, na maafisa wengine wa serikali wamezungumzia kwa kina juu ya kubadilika kwa jukumu la Marekani, wote wakisisitiza kuendelea kwa dhamira ya Marekani kuleta amani Iraq.