Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Machi 29, 2024 Local time: 15:55

Khartoum yakasirishwa na pendekezo la Juba


Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir na mwenzake wa Sudan Omar al Bashir baada ya mkutano na waandishi wa habari kabla ya Kiir kuondoka kwenye uwanja wa ndege wa Kharoum
Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir na mwenzake wa Sudan Omar al Bashir baada ya mkutano na waandishi wa habari kabla ya Kiir kuondoka kwenye uwanja wa ndege wa Kharoum

Sudan imeonya kwamba pendekezo hilo linaweza kuongeza hali ya wasiwasi baina ya nchi hizo mbili.

Mazungumzo ya amani kati ya Sudan na Sudan Kusini yaligonga mwamba Jumatano kufuatia pendekezo la Sudan Kusini linaloweza kuzuia Khartoum kufanya shughuli zozote kwenye machimbo ya mafuta ya Heglig mafuta. Katika majadiliano baina ya nchi hizo mbili yanyoendelea mjini Addis Ababa, Ethiopia, Sudan imeonya kwamba pendekezo hilo linaweza kuongeza hali ya wasiwasi baina ya nchi hizo mbili na hata kusababisha maadui hao wa zamani kurejea vitani. Sudan Kusini imependekeza eneo la kilomita 20 mraba lisilokuwa na wanajeshi kwenye mpaka baina yake na Sudan kama njia moja ya kulegeza hali ya wasiwasi. Khartoum mara moja ikapinga pendekezo hilo ikisema ni mbinu za kuzuia Sudan kufikia eneo la Heglig lenye utajiri wa mafuta. Waziri wa mambo ya nje wa Sudan Kusini Nhial Deng alisisitiza kuwa pendekezo la kuwa na eneo salama kati ya nchi hizo mbili linafuatana na azmio la hivi majuzi la baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalolenga kuzuia mlipuko wa vita baina ya nchi hizo mbili.

Naye msemaji wa wajumbe wa Sudan Omer Dahab alisema pendekezo hilo ni jaribio la kuzuia Khartoum kufikia machimbo ya mafuta ya Heglig. Heglig ni miongoni mwa machimbo machache ya mafuta yaliyosalia kwa Khartoum baada ya Sudan Kusini kuchukua maeneo mengi yenye raslimali za mafuta baada ya kupata uhuru wake yapata mwaka mmoja uliopita. Waziri wa Sudan Kusini Arop Deng anasema pendekezo la nchi yake litaiwezesha Khartoum kuendelea kuzalisha mafuta kutoka Heglig chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa. Lakini msemaji wa Sudan Omer Dahab anasema dai la Sudan Kusini linakiuka kabisa makubaliano ya mipaka na kuongeza uhasama kwenye mipaka baina ya nchi zao mbili. Lakini licha ya wasiwasi unaoendelea kujitokeza katika majadiliano baina ya nchi hizi mbili, wanadiplomasia na wapatanishi kutoka Umoja wa Afrika wanasema wangali na matumaini kuona mwelekeo mpya baada ya mazungumzo ya mawaziri kutoka nchi hizo. Kwa mujibu wa afisa wa ngazi ya juu, Sudan Kusini na Sudan kwa faragha zinasema hazitaki kuondoka kwenye majadiliano hayo bila kufikia makubaliano.

XS
SM
MD
LG