Wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu wiki hii wamethibitisha kesi kadhaa za COVID-19 katika kambi za Sudan kwa wakimbizi waliokimbia mapigano katika mkoa wa Tigray nchini Ethiopia. Shirika la kuhudumia wakimbizi katika Umoja wa Mataifa-UNHCR na kundi la msaada la Mercy Corps wanasema uingiliaji wa haraka unahitajika ili kuepusha janga la kibinadamu.
Mashirika ya misaada yaliripoti kesi nne za COVID-19 zilizothibitishwa, katika kambi ya Um Rakouba ya Sudan, kwa wakimbizi wa Ethiopia, wiki hii.
Kambi hiyo ni makazi ya watu 25,000 ambao wamewasili tangu Novemba mwaka jana, wanaishi katika mazingira ya kawaida sana, yenye msongamano mkubwa ambao unatoa fursa kwa virusi vya Corona kusambaa kwa urahisi.
Mercy Corps inaendesha kliniki ya afya katika kambi ya Um Rakouba, na inawatibu takribani wakimbizi 5,000. Mkurugenzi wa mkoa wa kundi hilo, Sean Granville-Ross alitoa wito wa hatua na uamuzi wa haraka uchukuliwe ili kuzuia kusambaa zaidi kwa virusi hivyo.
"Ni jambo linalotia wasi wasi sana kwetu sote-mazingira ya kwenye kambi, watu kutojiweza, idadi ya watu waliopo ambayo hufanya iwe vigumu kutekeleza masharti ya kutokaribiana kutoka mtu mmoja hadi mwingine. Na ukosefu wa vifaa, PPE, na vifaa vingine vya kutuwezesha kudhibiti mlipuko hu una kuwahudumia watu".
Watu hao wanne waliothibitishwa kuwa na COVID-19 wametengwa, anasema afisa wa UNHCR, Guilia Raffaelli.
Watu waliothibitishwa kuwa na kesi wametengwa na wanafuatilia mawasiliano yao huku wakisubiri matokeo. Shughuli nyingine zimesimamishwa, kama vile mawasiliano na jamii pamoja na vituo vyenye uhusiano na office, na fedha zaidi zinahitajika ili kujibu tatizo hili
Mamlaka ya Sudan walipokea misaada kutoka UAE nan chi nyingine za kiarabu, kusaidia wakimbizi wa Ethiopia hapo Disemba mwaka uliopita.
Waangalizi wa afya wanasema fedha zaidi zinahitajika, kutokana na mmiminiko kuongezeka na hatari inayoongezeka ya COVID-19.
Sudan imesajili zaidi ya kesi 23,000 zilizothibitishwa za COVID-19, tangu mwishoni mwa Oktoba, na zaidi ya vifo 2,000.
Wakati huo huo, serikali ya Sudan na mashirika ya misaada yamekamilisha maandalizi ya kuhamisha wakimbizi hao kwenda kwenye kambi mpya magharibi mwa Al-Qadarif. Serikali inasema hatua hiyo itaondoa wakimbizi kutoka eneo tete la mpakani na kuboresha usalama.