Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Juni 24, 2024 Local time: 04:20

Kenyatta akutana na Wakenya Marekani


Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta akihutubia kikao cha 69 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, New York Sept. 24, 2014.
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta akihutubia kikao cha 69 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, New York Sept. 24, 2014.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta anarejea Kenya baada ya ziara ya kufana na yenye shughuli nyingi nchini Marekani wiki hii. Jumatano Rais wa Kenya alitoa hotuba yake ya kwanza katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambapo alieleza kuwa nchi yake inabeba mzigo mkubwa wa kupambana na magaidi wa al-shabab miongoni mwa changamoto nyingine.

Rais Kenyatta alielezea juhudi za serikali yake za kupambana na ugonjwa hatari wa Ebola, ikiwa ni pamoja na kutoa msaada wa mamilioni ya fedha kusaidia Liberia kupambana na mlipuko wa ugonjwa huo.

Akiwa jijini New York, kiongozi wa Kenya alikuwa na mikutano mingine kando ya mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, akizungumzia changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa, juhudi za Kenya za kuhifadhi misitu pamoja na miradi mingine.

Alhamis jioni Bw. Kenyatta na mkewe Margaret walikutana na Wakenya wanaoishi New York na majimbo jirani ambapo aliwasihi kuwekeza nyumbani na kuwahimiza kutumia mitandao ya kijamii kuungana pamoja badala ya kupanda mbegu za chuki na ukabila kupitia mitandao hiyo.

Ijumaa jioni, rais Kenyatta, pamoja na mkewe walikutana na Wakenya wanaoishi Boston, Massachusetts na viunga vyake ambapo alieleza umuhimu wa kuheshimu katiba mpya ya nchi aliyosema ni katiba ya mwananchi inayopaswa kutekelezwa kikamilifu kufaidi Wakenya.

Wakati wa ziara yake Marekani, bwana Kenyatta alikutana na Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon, pamoja na rais wa Marekani Barack Obama na mkewe Michele. Wakati wa mkutano huo, Bw. Kenyatta alifuatana na mkewe Margaret.

XS
SM
MD
LG