Maelfu kwa maelfu ya wakenya walihudhuria leo sherehe kubwa za kutiwa saini kwa katiba mpya iliyotiwa saini katika viwanja vya Uhuru Park mjini Nairobi. Wakenya walipeperusha bendera na kushangilia kwa nguvu wakati katiba hiyo ikitiwa saini.
Rais Mwai Kibaki na Waziri Mkuu Raila Odinga na viongozi wengine wa serikali waliapishwa upya madarakani chini ya katiba hiyo mpya.
Sherehe hizo zilizoja kila aina shamrashamra zilihudhuriwa na viongozi na wawakilishi kutoka kote duniani, ikiwa ni pamoja na rais wa Sudan Omar Al-Bashir ambaye ana hati ya kukamatwa kutoka kwa mahakama ya kimataifa ya makosa kijinai.
Rais Kibaki alisema hiyo "Ni siku kubwa sana kwa Kenya," na siku muhimu kuliko zote tangu Kenya ipate uhuru wake mwaka 1963. Waziri Mkuu Raila Odinga aliuambia umati uliohudhuria kuwa wanashuhudia "kuzaliwa upya kwa umoja wa kitaifa."