Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Desemba 08, 2022 Local time: 22:08

Kenya yazindua bima ya afya kwa raia wake wote


Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta

Serikali ya Kenya imezindua mpango wa kutoa bima ya afya kwa kila raia wake ili kuwawezesha kupata matibabu kwa bei nafuu.

Rais wa nchi hiyo Uhuru Kenyatta amesema mpango huo ni sehemu ya agenda zake nne za maendeleo kwa ajili ya raia wote wa Kenya.

Uzinduzi huo unajiri baada ya miaka miwili ya kufanyiwa majaribio yaliyokuwa yakiendelea katika miji minne ya Kisumu, Machakos, Nyeri na Isiolo.

Serikali ya Kenya imesema kwamba imejitolea kufanya uwekezaji wa kimkakati katika sekta ya afya ili kuhakikisha kwamba raia wote wa nchi hiyo wanapata huduma muhimu za afya wanazohitaji ifikapo mwaka 2022.

Raia wa Kenya milioni moja kutoka jamii maskini watasajiliwa kwa njia ya digitali katika awamu ya kwanza.

Katika mkutano wa wadau mjini Mombada, uliowaleta Pamoja magavana na viongozi wengine wa serikali kuu ili kuthathmini hatua muhimu zilizofikiwa katika mpango wa majaribio, imeelezwa kwamba kuna nafasi kubwa sana kwa mpango huo kutekelezwa kwa haraka katika majimbo yote ya Kenya, 47.

Rais Uhuru Kenyatta ametoa wito kwa kila raia wa Kenya kuunga mkono mpango huo, akitoa mwito kwa bunge kupitisha kwa haraka sheria kuulinda.

"Msicheleweshe mpango huu kwa mijadala isiyofaa. Sote tunajua tunakotaka kwenda. Huu sio wakati wa kutuonesha uwezo wako katika mijadala.” Amesema Uhuru Kenyatta.

Kenyatta ameonya wasimamizi wa mpango huo kutofuja fedha za umma zinazotakiwa kufanikisha utekelezwaji wake.

“tuna nafasi ya kurekebisha tatizo mara moja na mwisho kabisa. Ikiwa wale waliopewa jukumu la kushughulikia fedha hizi hawatafanya hivyo kwa uangalifu na tahadhari, watajuta kwa maisha yao yote.”

Kufikia sasa, kuna karibu watu milioni 22 ambao wamesajiliwa kwa mfumo wa bima ya afya ya kitaifa NHIF, ambayo wasimamizi wake wanasema watatumia taarifa za waliosajiliwa kuharakisha ufanisi wa mfumo mpya ambao umezinduliwa.

Imetayarishwa na mwandishi wetu wa Nairobi, Kennedy Wandera.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG