Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Septemba 24, 2023 Local time: 16:25

Kenya, Djibouti zashindwa kupata kura za kutosha kwa kiti cha Baraza la Usalama, UN


Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Kenya Jumatano ilipata kura 133 dhidi ya Djibouti iliyozoa kura 78, na hivyo nchi zote mbili kushindwa kupata theluthi mbili ya kura zote, kama inavyohitajika, ili kushinda kiti kisicho cha kudumu kwenye baraza la Usalama la Umoja wa mataifa.

Nchi hizo mbili zinatarajiwa kuingia kwa duru ya pili ya uchaguzi huo Alhamisi, ili kumtafuta mshindi, atakayeshikilia nafasi hiyo kwa miaka miwili.

Mexico. India, Ireland na Norway zilichaguliwa lakini sasa itabidi mataifa yote 193 ya Umoja huo, yakutane tena ili kujaza pengo lililobaki baada ya Kenya, ambayo ilikuwa imepata uungwaji mkono wa Umoja wa Afrika, kutopata idadi ya kura iliyohitakjika.

Djibouti ilikataa kuheshimu uamuzi wa Umoja wa Afrika na kuamua kwendelea na mchakato wa kampeni ya kutafuta uungwaji mkono kutoka kwa nchi mbalimbali.

Kwa sasa, Afrika inawakilishwa na Niger, Tunisia na Afrika Kusini kwenye baraza hilo. Hata hivyo, awamu ya Afrika Kusini inafika kikomo mwishoni mwa mwaka huu, na nafasi yake ndiyo inayopiganiwa na Djibouti na Kenya.

Katika maeneo mengine duniani, Canada ilishindwa na Ireland na Norway kwenye uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali uliopekea Ireland kuomba usaidizi wa mwanamziki maarufu, Bono, na kupeleka wajumbe wa Umoja wa mataifa kwenye onyesho lake nchini Canada, na pia kupleeka wengine kwenye show ya mwanamuziki mwingine maarufu Celine Dion ili kuwarai kupiga kura.

Mexico na India zilichaguliwa bila kupingwa. Mataifa mapya kwenye baraza hilo lenye wajumbe 15 yataanza muhula wao wa miaka miwili Januari mosi mwaka 2021.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ni chombo muhimu zaidi kwenye mfumo wa Umoja huo kwani lina nguvu za kufanya maamuzi yenye uzito mkubwa kimataifa.

Baraza hilo lina wanachama wa kudumu watano: Marekani, China, Russia, Ufaransa na Uingereza, ambao kila mmoja ana kura ya turufu.

-Imetayarishwa na Harrison Kamau, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG