Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Oktoba 08, 2024 Local time: 20:57

Kenya yaongeza kiwango cha bajeti yake ya 2023/24 kwa shilingi bilioni 200


Rais wa Kenya William Ruto
Rais wa Kenya William Ruto

Serikali ya Kenya imeongeza kiwango cha bajeti yake ya mwaka 2023/24 ya shilingi trilioni 3.67 kwa shilingi bilioni 200 hadi shilingi trilioni 3.95 kutokana na malipo ya kiwango cha riba kwa madeni ya nchi na kushuka kwa thamani ya shilingi ya Kenya, Kamati ya bunge ya bajeti imetangaza Jumatano.

Kamati hiyo inasema kuwa malipo ya kiwango cha riba kwenye madeni ya nchi yameongezeka na shilingi ya Kenya imeshuka thamani, hivyo bajeti ya mwaka huu ya shilingi trilioni 3.67 itaongezeka kwa shilingi bilioni 200 hadi shilingi trilioni 3.95.

“Ili kutolegeza kasi ya ulipaji wa madeni ya serikali, shilingi bilioni 145 za ziada zimetengewa ulipiaji wa riba kwenye deni la umma”, amesema mwenyekiti wa kamati hiyo Ndindi Nyoro.

Mdhibiti wa bajeti Margaret Nyakang’o akiwa mbele ya kamati ya ubinafsishaji amefichua kuwa ongezeko la makadirio ya nyongeza ya deni la nje kwa kiasi cha shilingi bilioni 216 hadi shilingi bilioni 839.1 kutoka shilingi bilioni 622.4 kwa kiasi fulani limechangiwa na kushuka thamani kwa shilingi ya Kenya.

Kiwango cha ubadilishaji fedha kilikuwa shilingi 136.0 kwa dola ya Kimarekani kufikia Aprili 30 mwaka huu kabla ya kushuka hadi shilingi 151.4 tarehe 7 Novemba mwaka huu, hii ikimaanisha kuna hasara ya asilimia 11.3 ya thamani ya shilingi ya Kenya.

Serikali ya rais Ruto, kwenye bajeti yake ya mwaka 2023/24 tayari ilitaraji kuziba mapungufu ya shilingi bilioni 718, sawa na 4.4% ya pato la taifa kwa kukopa shilingi bilioni 131 kutoka vyanzo vya kigeni, sawa na asilimia 0.8% ya pato la taifa, na shilingi bilioni 586 kutoka kwa wakopeshaji wa ndani, sawa na 3.6% ya pato la taifa.

Vile vile, serikali yake kupitia bajeti hiyo iliyosomwa Juni, ilitaraji kutafuta mapato ya ziada ya ushuru ya angalau shilingi bilioni 211 kufadhili bajeti hii ya kwanza ya utawala wa Ruto, ambayo ni kubwa zaidi katika historia Kenya.

Charles Karisa, mchambuzi wa masuala ya uchumi nchini Kenya anasema” kuongezwa kwa bajeti hii kuna athari kubwa kwa ukuaji wa uchumi na raia wa Kenya wanaoendelea kukabiliwa na hali ngumu ya maisha wataathirika zaidi.”

Karisa anakariri kuwa “kuongezeka kwa kiwango cha ulipaji wa riba kwa madeni, kutakwamisha maendeleo ya nchi na kufanya ufikiaji wa huduma muhimu kuwa mgumu.”

Tayari serikali imetangaza kupunguza matumizi ya fedha zinazoelekezwa kwenye ufadhili wa mandeleo kwa shilingi bilioni 42 lakini ikaongeza kiwango cha bajeti yake kugharamia malipo ya riba yanayotokana na kile inachokitaja kuwa ni kuongezeka kwa kiwango cha riba duniani na kushuka kwa thamani ya shilingi kwani madeni mengi ya Kenya yanatokana na dola ya Kimarekani.

Ripoti imeandaliwa na Kennedy Wandera

Forum

XS
SM
MD
LG