Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Machi 29, 2024 Local time: 09:31

Kenya yakanusha kuingiza silaha Sudan Kusini


Mwanajeshi wa Sudan Kusini.
Mwanajeshi wa Sudan Kusini.

Serikali ya Kenya Jumatano imekanusha vikali madai ya kuingiza silaha nchini Sudan Kusini.

Taarifa iliotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Monica Juma, imesema Jumatamo kwamba madai hayo ni ya kupotosha na kwamba hayachangii katika mchakato wa kutafuta amani katika nchi hiyo changa zaidi duniani.

Madai yaliotolewa na Adama Dieng, Mshauri Maalum wa Umoja huo kuhusu Udhibiti wa mauaji ya halaiki yaliishitua Kenya na kupelekea kutoa tamko hilo.

Dieng alisema kwamba Kenya na Uganda ni baadhi ya mataifa ya Afrika Mashariki yanayoingiza silaha nchini Sudan Kusini.

Akizungumza na kipindi cha Voice of America, Sudan in Focus mwezi uliopita, Dieng alieleza kuwa Kenya na Uganda zinaendeleza mapigano nchini Sudan Kusini.

"Ijapokuwa jukumu ni kulinda umma Sudan Kusini, jukumu sasa ni la serikali ya Sudan Kusini; jukumu la kuzuia uovu ni la kikanda na kimataifa," alisema mjumbe huyo..

Afisa huyo wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa aliongeza kuwa silaha nyingi za maangamizi zinaingia Sudan Kusini kutoka Kenya na Uganda.

“Ni kweli kuwa silaha nyingi na risasi zinaingia Sudan Kusini kupitia Kenya na Uganda," aliongeza Adama Dieng.

Na jana wakati akitoa ripoti kwa Baraza la Usalama, Katibu Mkuu wa Umoja huo Antonio Guterres, alisisitiza kuwa huenda machafuko yakaendelea kushuhudiwa nchini Sudan Kusini kwa sababu kuna baadhi ya mataifa jirani yanayoendeleza mzozo nchini humo.

Haya yanajiri wakati Kenya imetoa ujumbe mkali kupuuzilia mbali matamshi ya mjumbe huyo kuwa Kenya inahujumu upatikanaji wa amani mjini Juba.

Taarifa ya liotolewa na Waziri Juma ilisema kuwa Kenya itaendelea kufanikisha juhudi za kupatikana kwa amani katika taifa hilo ambalo limekumbwa na machafuko kutokana na mzozo wa kisiasa kati Rais wa taifa hilo Salva Kiir Mayardit na kiongozi wa upinzani Riek Machar yaliyoibuka Desemba 15, 2013.

“Madai ya afisa wa ngazi ya juu wa umoja wa mataifa kwamba Kenya inahusika katika biashara ya kuingiza silaha nyingi Sudan Kusini ni ya kushangaza na kupotosha na pia hayana ithibati yoyote na yanajiri wakati ambapo mataifa yote wanachama wa IGAD yameanza mchakato mkali wa kuimarisha Mkataba wa Makubaliano wa kutafuta suluhu ya mgogoro wa Sudan Kusini (ARCSS) uliotiwa sahihi Agosti 2015.”

Kenya pia imesisitiza kuwa haitavumilia kitendo chochote kinachohujumu upatikanaji wa amani nchini Sudan Kusini ‘ili kufanikisha majukumu yake ya kimataifa. Serikali ya Kenya haitakivumilia kitendo chochote cha machafuko dhidi ya majirani zake,nchi jirani au serikali jirani katika ukanda wake. Mtu yeyote au kikundi chochote au watu wanaohujumu mchakato wa upatikanaji amani, awe raia wa Kenya au kigeni, watachunguzwa na kupitishwa kwenye utaratibu ufaao,”aliongeza Dkt Juma.

Hata hivyo, akizungumza na Sauti ya Amerika siku ya Jumatano, Dkt Mumo Nzau, mtaalam wa masuala ya kidiplomasia na Uongozi kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi, ameeleza kuwa matamshi yaliyotolewa na Umoja wa Mataifa hayaathiri kwa vyovyote juhudi za Kenya kufanikisha upatikanaji wa amani nchini Sudan Kusini.

“Haiwezi maanake hata Sudan Kusini wanajua Kenya haiwezi kufanya mambo kama yale. Sudan Kusini iko na sisi, Sudan Kusini iko na nchi zake za karibu,Uganda na Tanzania na nchi zetu za Afrika Mashariki, Ethiopia ikiwemo. Kila nchi inatakia Sudan Kusini ile hali ya amani na hali ya kujenga nchi yao,’’alieleza Dkt Nzau.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Kennedy Wandera, Kenya.

XS
SM
MD
LG