Wanajeshi wa Kenya wameingia ndani zaidi ya Somalia kusini baada ya kuvuka mpaka kupambana na kundi la wanamgambo wa al-Shabab.
Wakazi wa eneo hilo walisema Jumatatu kwamba majeshi ya Kenya , yakifuatwa na magari yenye uwezo wa kuzuia risasi yalikuwa karibu na kijiji cha Qoqani, ambacho kilikimbiwa na al-Shabab Jumamosi.
Al-Shabab wameapa kupambana na majeshi ya Kenya na kuwataka wasomali wote kujilinda dhidi ya adui. Kuna ripoti kwamba wanamgambo hao wameteka nyara na kupanga magari makubwa mengi katika eneo la lower Shabelle karibu na mji mkuu Mogadishu.
Maafisa wa Kenya wanawalaumu al-Shabab kwa utekaji nyara wa hivi karibuni ambao unaweza kuhatarisha jina la Kenya kama sehemu salama ya utalii.
Msemaji wa al-Shabab Sheikh Ali Dheere amekaririwa katika vyombo vya habari kadha akisema serikali ya Kenya imetangaza vita dhidi yake na kwamba kundi hilo litachukua hatua za kushambulia maeneo yatakayoathiri uchumi wa Kenya hasa katika sekta ya utalii.