Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Juni 16, 2024 Local time: 06:19

Baraza: Matokeo ya mtihani wa sekondari Kenya ni uhalisia wa uwezo wa wanafunzi


Waalimu wakiwa nje ya majengoya bunge Nairobi, Kenya Septemba 2011.
Waalimu wakiwa nje ya majengoya bunge Nairobi, Kenya Septemba 2011.

Ni heri tuwe na alama za chini lakini ambazo ni halisia kuliko alama za juu za A ambazo si halisia.

Matokeo ya mtihani wa shule za sekondari nchini Kenya yamewashtusha wanafunzi, wazazi na waalimu ambao walikuwa na matarajio makubwa.

Akizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya VOA, mtaalamu wa elimu nchini Kenya, Tomkin Baraza amesema shule kadhaa zilikuwa zimezoea kupata alama za juu na hivyo kushuka daraja kwa idadi kubwa ya wanafunzi mashuleni kumewaacha wamepigwa na butwaa.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotangazwa na Waziri wa Elimu, Dr. Fred Matiang’i ni wanafunzi 141 waliopata tija ya juu ya wastani wa alama A ukilinganisha na mwaka jana ambapo wanafunzi 2636 walifaulu kwa wastani huo.

Tomkin Baraza, mtaalamu wa elimu Kenya anasema hatua alizochukua waziri wa elimu zinafaa kupongezwa.

“Ukilinganisha na hali ya awali pale ambapo tulikuwa na hali ya utepetevu na uchakachuaji katika mitihani ya Kenya,” alisema.

“kwa vile Dr. Matiang’i aliweza kutoa matokeo kwa muda mfupi kwani ikumbukwe karatasi ya mwisho ilimalizika kusahihishwa siku ya krismas tarehe 25 na matokeo yalikuwa tayari siku ya pili,” alipongeza.

Alisema hiyo ni hatua kubwa kwa Kenya kwani zamani ilikuwa inachukua miezi mitatu ndipo matokeo yaweze kutolewa.

“Uhalisia huu wa matokeo utawafanya wanafunzi waongeze bidii kwani wanafahamu mchuma juani hulia kivulini,” alisema.

Alipo ulizwa juu ya matokeo hayo alisema kwake yeye anayaona ni mazuri.

“Haya matokeo kulingana na mimi ni mazuri sana na kuwa hadhi ya elimu imeimarika na sio kuwa imeshuka,” alisisitiza.

“Ni heri tuwe na alama za chini lakini ambazo ni halisia kuliko alama za A nyingi lakini sio halisia.”

Hii ndio hali halisi ya kiwango cha elimu nchini Kenya. Kila alama iwe C au D hiyo ndiyo waliostahili watahiniwa.

Kwa hiyo ataenda kutafuta kozi inayolingana na ile alama na kuifanya vizuri.

Ikilinganishwa na zamani wengi walikuwa wanapata alama A na anakwenda kufanya kozi fulani anafika katikati anaacha anaanza kuchukua kozi nyingine hiyo si picha nzuri.

Mabadiliko yameweza kulisafisha baraza la mitihani NEC lililokuwepo. Kwasababu miaka iliyopita mitihani mingi ilikuwa inavuja na wanauziwa watu.

Alisafisha huko na kuhakikisha kwamba vituo vya kusahihisha mitihani viko karibu na jiji la Nairobi, alisema mtaalamu huyo.

“Serikali ilikuwa ina hakikisha kwa siku zote kumi na tano za kusahihisha mitihani kwamba kazi inafanyika kwa njia ambayo inastahili na hakuna mtu yeyote anaweza kuja ahonge mtu kwa ajili ya kumuongezea alama na hivyo kubadilisha matokeo,” alisema.

Wakati huo huo mwalimu Ota Sinifu wa Mombasa anasema matokeo yameshuka kwa sababu kuna mikakati ya waziri wa elimu, kuhakikisha kwamba wizi wa mitihani unakomeshwa.

“Sisi kama waalimu tunashuku kwamba miaka ya awali wizi wa mitihani ulikuwa umekithiri,” alisema.

Alimpongeza waziri kwa kuchukua hatua za kuziba mianya ya wizi huo wa mitihani.

“Matokeo ya mwaka huu yanaonyesha uhalisia wa uwezo wa wanafunzi, kwani siku za nyuma mwanafunzi alikuwa anapata alama ya A ambayo ilikuwa ya juu mno kupita uwezo wake,” alisema.

“Hatuwezi kuridhika kwamba ni matokeo mazuri, ni matokeo mabaya kama alivyosema rais mwenyewe, na kuthibitishwa na mkuu wa kitengo cha Teachers Service Commission,” alisema.

“Sisi kama waalimu tumepewa changamoto kubwa, hii ni changamoto kwetu kuwa tuongeze bidii, na mwaka huu kuna mabadiliko makubwa yamefanyika katika wizara ya elimu,” alisisitiza.

XS
SM
MD
LG