Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Aprili 16, 2024 Local time: 12:38

Kenya: Viongozi wa Kiislam wamshauri rais kutomchukulia hatua jaji Chitembwe


Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta

Viongozi wa dini ya Kiislamu nchini Kenya wamemshauri rais wa taifa hilo Uhuru Kenyatta kutomchunguza na kumuondoa kazini Jaji wa Mahakama Kuu Said Juma Chitembwe kwa tuhuma za utovu wa nidhamu na doa la kimaadili.

Viongozi hao chini ya mwavuli wa Baraza la Kitaifa la Ushauri la Waislamu wanadai kuwa Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) haikumpa nafasi na muda wa kutosha wa kujitetea dhidi ya madai yaliolimbikizwa dhidi yake.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari Rais Kenyatta anastahili kuunda jopo hilo ndani ya siku kumi na nne baada ya kupokea hati za JSC.

Wakati jaji Said Juma Chitembwe akisubiri hatma yake kuamuliwa na jopo lililoundwa na rais Kenyatta, ndani ya kipindi cha siku kumi na nne baada ya kupokea hati za ushahidi kutoka kwa tume ya huduma za mahakama kwa mujibu wa kifungu cha sheria cha 168(b), viongozi wa dini ya kiislamu sasa wanadai jaji huyo anaandamwa.

Mwenyekiti wa baraza hilo Sheikh Juma Ngao amedai kuwa jaji Said Juma Chitembwe hajapewa muda wa kutosha kujitetea.

Aidha, Sheikh Ngao anaeleza kuwa ombi lake, tume ya huduma za mahakama, inastahili kufungua upya kipindi kingine cha jaji Chitembwe kuwasilisha ushahidi wa kina alionao kuhusu kesi inayomkabili.

Jaji Said Juma Chitembwe, mwenye umri wa miaka 55, yuko kwenye hatari ya kuondelewa afisini baada ya tume hiyo ya huduma za mahakama nchini Kenya, Jumatano wiki iliyopita kupendekeza rais Kenyatta kubuni jopo la kuchunguza tabia na mienendo yake.

JSC, katika hati ya ombi kwa rais, inasema kuwa imeridhishwa na ushahidi uliowasilishwa mbele yake na madai hayo yanafichua sababu za kuondolewa Chitembwe kazini na imeazimia kumtaka rais Kenyatta kumfukuza kazi kwa mujibu wa vigezo vya sheria, kwa tuhuma za utovu wa nidhamu na doa la kimaadili kutokana na msururu wa kanda zinazomnasa akihusishwa na tuhuma za ufisadi.

Jaji Chitembwe, alikuwa mmojawapo wa wagombea wanaowania nafasi ya Jaji Mkuu kumrithi David Maraga aliyestaafu, baada ya kutimiza umri wa miaka 70 ambao ni ukomo wa kuhudumu kuwa jaji mkuu nchini Kenya.

Lakini alibwagwa kwenye ugombea i huo na Martha Koome ambaye aliteuliwa kuwa jaji mkuu wa 15 na mwanamke wa kuanza kuwahi kuishika nafasi hiyo nchini Kenya, likiwa taifa huru.


Imetayarishwa na mwandishi wetu Kennedy Wandera, Nairobi, Kenya

XS
SM
MD
LG