Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Aprili 24, 2024 Local time: 11:35

Kenya: Ruto amjibu Rais Kenyatta, asema hatajiuzulu


Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta (Kushoto) na naibu wake William Ruto.
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta (Kushoto) na naibu wake William Ruto.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta anamtaka naibu wake, William Ruto, kujiuzulu kutoka serikalini iwapo haridhishwi na utendakazi wake badala ya "kuendelea kutumia rasilimali za serikali wakati anaendelea kuipinga."

Kenyatta, akizungumza na jukwaa la wahariri nchini humo Jumatatu alieleza kuwa Ruto anastahili kuamua iwapo anataka kuitumikia serikali au kama anataka kuendeleza azma yake ya kuwania urais mwaka ujao.

Hata hivyo, Ruto Jumanne alionekana kumjibu rais Kenyatta kwa kueleza kuwa japo anaomba radhi, wasiomuelewa wanastahili kumvumilia.

Kenyatta alifungua roho na kuelezea kwa kina hulka ya naibu wake katika serikali. Alivyofanya miezi ya nyuma, Bw Kenyatta alikumbusha Bw Ruto kuwa anastahili kuamua, kusalia serikalini au kuondoka ili kuendeleza azma yake ya kuwania urais mwaka 2022.

Kenyatta ashauri makamu wake ajiuzulu
please wait

No media source currently available

0:00 0:03:22 0:00

“Kwa kweli litakuwa jambo la heshima kuwa iwapo hufurahii unajiondoa na kujiuzulu na kuwaruhusu wanaotaka kuendelea kufanya hivyo na kisha upeleke ajenda yako kwa raia hivyo ndivyo inavyotokea katika demokrasia yoyote ya kawaida, huwezi kwa upande mmoja kusema siendi na kwa upande mwingine unasema sikubaliani, lazima uamue, lazima uwe na falsafa katika jaribio hilo,” alisema Kenyatta

Rais huyo alisema kuwa Ruto hastahili kuendelea kutumia rasilimali za serikali wakati anaendelea kuipinga serikali hiyo. Aidha, Kenyatta alisisitiza kuwa hafahamu kilichosababisha uhusiano wake na naibu wake kudorora kiasi hicho na haelewi kubadilika kwa msimamo wa naibu wake.

“Sijui ni nini kimetukia isipokuwa ukweli ni kwamba labda anajaribu kupata msingi wa siasa zake za baadaye ambayo ni haki yake ya kimsingi, sijawahi kumnyima hiyo na yuko huru kufanya hivyo lakini nahisi ni vibaya jinsi anavyofanya, kwa kwenda kinyume na serikali hiyo hiyo anayotumikia, nadhani ni makosa,” alisema.

Jumanne Ruto ameonekana kama kumjibu Bw Kenyatta kwa kuomba radhi na kusema kuwa wasiomuelewa wanastahili kumvumilia lakini hawezi kukatiza azma yake.

"Ndiyo nasema kwa wale ambao wanaoona nimewakosea nawaomba msamaha. Lakini nimeamua kwamba sina nafasi ya kurudi nyuma na sina starehe ya kusarenda," alisema naibu wa Rais Ruto.

Franklin Bett, aliyehudumu kuwa waziri katika serikali ya rais wa pili hayati Daniel Arap Moi na rais mstaafu Mwai Kibaki ameeleza kuwa mvutano huu hufai na kumnyooshea Bw Ruto kidole cha lawama.

Je, utendakazi wa serikali unaweza kuathirika kwa kiwango gani? Swali hili nimemuuliza Profesa Chacha Nyaigoti Chacha, mfuatiliaji wa siasa na uongozi nchini Kenya

Bw Bett anaeleza kuwa Kenyatta na Ruto walikosea kwa kubuni baraza la mawaziri lenye idadi sawa kila mmoja, hii iliashiria uwezo sawa madarakani.

Kwa mujibu wa katiba ya Kenya kifungu cha 150, Rais Kenyatta hawezi kumfuta kazi naibu wake, lakini Ruto anaweza kujiuzulu, au kuondolewa afisini kupitia hoja ya bunge kukosa imani naye inapothibitishwa kuwa hana uwezo wa kiakili kutekeleza majukumu yake, au amevunja sheria za nchi kwa kutekeleza uhalifu.

Aidha, Kenyatta amesisitiza kuwa kuharamishwa kwa ufanyikaji wa marekebisho ya katiba na mahakama ya rufaa ni pigo kwa taifa na kwamba mahakama ilipotoshwa na misingi ya kisiasa, lakini ataheshimu mfumo wa kisheria.

-Imetayarishwa na Kennedy Wandera, VOA, Nairobi

XS
SM
MD
LG