Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Machi 05, 2024 Local time: 06:51

M-Pesa yanasa polisi Kenya, 63 watimuliwa


Msongamano wa magari barabarani Nairobi. REUTERS/Goran Tomasevic - RTR4WDE5
Msongamano wa magari barabarani Nairobi. REUTERS/Goran Tomasevic - RTR4WDE5

Maafisa wa ngazi za juu 63 wa jeshi la polisi nchini Kenya wamefukuzwa kazi katika juhudi za kusafisha jeshi hilo kutokana na madai ya rushwa. Miongoni mwa waliofukuzwa ni pamoja na aliyekuwa msemaji wa jeshi hilo Masoud Mwinyi.

Maafisa wa cheo cha SSP 28 pamoja na ASP watatu wamefukuzwa, kulingana na Mwenyekiti wa tume ya huduma za polisi Johnston Kavuludi. Amesema uchunguzi wa maafisa wengine 29 bado unaendelea.

Kavuludi amesema maafisa waliofukuzwa wamekutwa na makosa mbali mbali ikiwa ni pamoja na rushwa, ukiukaji wa haki za binadamu, vitendo vya kihalifu na makosa mengineyo.

Katika uchunguzi huo iligundulika kupitia akaunti za kutuma pesa za M-Pesa kwamba maafisa wa kuongoza magari barabarani wanatuma kiwango maalum cha fedha kwa wakubwa wao kila siku kupitia M-Pesa. Hali hiyo iliashiria kwamba polisi hao wanatumwa na maafisa wa ngazi za juu kukusanya fedha barabarani kutoka kwa waendesha magari.

Kwa muda mrefu madereva Nairobi na miji mingine wamekuwa wakilalamika kuwa wanasumbuliwa na kudaiwa faini na polisi barabarani katika hali inayoonyesha kuwa fedha hizo haziendi katika mfuko wa serikali.

XS
SM
MD
LG