Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Februari 09, 2023 Local time: 02:34

Polisi yakanusha ripoti za ugaidi katika madrasa Mombasa


Wazazi wakiwa nje ya mahakama ya watoto Mombasa kuwatambua watoto wao

Polisi nchini Kenya imekanusha ripoti kuwa ilivamia madrasa moja nje kidogo ya Mombasa Jumanne katika operesheni ya kukabiliana na ugaidi, kama ilivyoripotiwa katika vyombo vingi vya habari.

Afisa anayesimamia ulinzi wa watoto katika idara ya upepelezi wa makosa ya jinai nchini Kenya Grace Ndirangu ameiambia VOA Swahili, kuwa oparesheni yao ilinuia kuokoa wanafunzi hao wa shule ya Al Madrasatul Falan iliyopo Likoni, Mombasa kufuatia madai kwamba watoto hao wananyanyaswa.

Ndirangu alikashifu ripoti za vyombo vya habari ndani na nje ya kwa kupotosha maelezo kwamba oparesheni hiyo ililenga ugaidi na ulanguzi wa watoto.

“(Operesheni) ilihusisha unyanyasaji wa watoto. Hakukuwa na FBI wala Scotland Yard. Tuliita watu wa balozi kwa sababu kuna watoto waliletwa na wazazi wao kutoka nchi za nje,” alisema Ndirangu.

Nao viongozi wa kidini, wasimamizi na wazazi wa madrasa hiyo wamekana madai yaliyotolewa awali na pia kukosoa vyombo vya habari kwamba vimetia chumvi taarifa zao.

Ndirangu amesema kuwa wanafunzi 20 wenye uraia wa mataifa ya kigeni zikiwemo Marekani, Uingereza, Norway, waliletwa katika madrasa hiyo na wazazi wao kwa hiari.

Kelvin Lay, kutoka kitengo cha kukabiliana na ulanguzi wa watoto, kwenye ubalozi wa Uingereza nchini Kenya, akiwa miongoni mwa waliofika katika madrasa hiyo Jumanne, amesema kuwa hakukua na visa vya ugaidi kwenye madrasa hiyo.

Wasimamizi wa madrasa hiyo ambao hawakutaka kuzungumza na wanahabari wamekosoa ripoti zilizochapishwa katika magazeti ya Kenya, wakisema zinalenga kuwaharibia sifa.

Upande wao wazazi wa madrasa wamekana shutuma kwamba watoto wao walikuwa wanachapwa sana shuleni hapo bila wao wazazi kulalamika.

Hadi Jumatano alasiri ripoti za polisi zinasema watoto 85 kati ya 95 waliondolewa madrasa hapo walikuwa wamekabidhiwa kwa wazazi wao, huku kumi wakisubiri kutambuliwa katika kituo cha kuhifadhi watoto Mombasa.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG