Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Julai 15, 2024 Local time: 08:13

Uzembe wa madaktari wasababisha baadhi ya wagonjwa kupoteza maisha Kenya


Wagonjwa wakiwa katika foleni kusubiri kupatiwa huduma kwenye kliniki ya Blue House jijini Nairobi.
Wagonjwa wakiwa katika foleni kusubiri kupatiwa huduma kwenye kliniki ya Blue House jijini Nairobi.

Uzembe wa madaktari kutoa huduma ya dharura kwa wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo umezua mjadala mkali nchini Kenya, baada ya kuripotiwa uzembe katika kifo cha Alex Madaga aliyekosa kupatiwa huduma ya dharura na kulazimika kukaa ndani ya ambulensi kwa takriban saa 18.

Huku hospitali ya Kenyatta na Coptic zikitakiwa kuelezea ni kwa nini Alex Madaga alipoteza maisha yake kwa kukosekana kwa huduma ya dharura, jamii mbili jijini Nairobi pia zinaomboleza vifo vya jamaa zao waliopoteza maisha yao mikononi mwa hospitali zilizogoma kutoa huduma ya dharura kunusuru wapendwa wao na hata nyingine kuzembea kazini.

Anne, ambaye hataki jina lake halisi litumike, anasema kuwa alimpoteza mpwa wake kwa njia ya kutatanisha katika hospitali ya Kenyatta. Anaeleza kukasirishwa kwake kutokana na uzembe wa wahudumu wa hospitali hiyo.

Salma Ali Nassir, mkazi wa Nairobi, anaelezea kumpoteza mama yake mzazi kutokana na uzembe wa madaktari wa hospitali ya Nairobi West. Salma anaeleza kuwa aliamua kwenda hospitali ya Nairobi West tu wakati walipokosa huduma ya dharura katika hospitali ya Avenue iliyopo Parklands jijini Nairobi.

Hata hivyo, hatua ya kuwafikia madaktari katika baadhi ya hospitali za binafsi mjini humo kuelezea jinsi wanavyotoa matibabu ya dharura ziligonga mwamba kwani walionekana kuogopa kuzungumza kutokana na utata unaozingira hospitali za Kenyatta na Coptic kuhusu kifo cha Alex Madaga.

Kwa mujibu wa kanuni za afya za maadili ya kitaaluma na nidhamu nchini Kenya, mgonjwa yeyote anayehitaji matibabu ya dharura hafai kunyimwa au kucheleweshewa kupatiwa huduma hiyo.

Je, hospitali za Kenya zinatibu vipi wagonjwa walio katika hali mahututi? Fred Majiwa, Afisa wa shirika la St. John’s Ambulance anaelezea taratibu zote zinazohitajika katika kuhudumia wagonjwa mahututi.

please wait

No media source currently available

0:00 0:07:06 0:00
Kiungo cha moja kwa moja

Bwana Majiwa pia anaeleza kuwa sheria mpya za matibabu ya rufaa zilizoidhinishwa hivi majuzi zimeleta mabadiliko makubwa ambayo wakati mwingi yanachangia pakubwa kukosekana kwa huduma ya dharura kwa wagonjwa.

Kizingiti kingine ambacho pia kimeshuhudiwa na mashirika ya ambulensi nchini ni watumiaji wa barabara jijini Nairobi kuonekana kutozipisha ambulensi hizo kuwaharakisha wagonjwa hospitalini.

Kwa sasa familia ya Alex Madaga na familia nyingine ambazo tumeziangazia katika makala hii bado zinasubiri maelezo kuhusu vifo vya wapendwa wao.

XS
SM
MD
LG