Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Juni 19, 2024 Local time: 01:41

Maathai ataka wakenya waunge mkono ICC


Mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu-ICC, Luis Moreno-Ocampo.
Mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu-ICC, Luis Moreno-Ocampo.

Mshindi wa Tuzo ya Nobel, Wangari Maathai, anawasihi viongozi wa jumuia za kiraia nchini Kenya kuunga mkono uchunguzi wa mahakama katika uhalifu dhidi ya ubinadamu uliotokea kwenye uchaguzi uliokuwa na utata mwaka 2007.

Wiki moja kabla ya mkutano wa kimataifa kuanza nchini Uganda kupitia tena mamlaka ya mahakama ya kimataifa ya uhalifu, mshindi wa Tuzo ya Nobel, Wangari Maathai, anawasihi viongozi wa jumuia za kiraia nchini Kenya kuunga mkono uchunguzi wa mahakama katika uhalifu dhidi ya ubinadamu uliotokea kwenye uchaguzi uliokuwa na utata mwaka 2007.

Mshindi wa Nobel Wangari Maathai.
Mshindi wa Nobel Wangari Maathai.

Wangari Maathai alizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari ulioandaliwa na Nobel Women’s Initiative, katika kuunga mkono mkutano wa kutathmini mahakama ya uhalifu wa kimataifa, wiki ijayo mjini Kampala. Alisifia kazi ya mahakama hiyo na mwendesha mashtaka wake, Luis Moreno-Ocampo, kuwaelezea na kuwachukulia hatua walioshiriki kwenye mapigano ya kikabila ambayo yaliibuka nchini Kenya mwaka 2008.

Baada ya wapinzani wakuu, Rais Mwai Kibaki na Waziri Mkuu Raila Odinga kushutumiana kila mmoja kuiba kura wakati wa upigaji kura ya urais mwaka 2007, wafuasi kutoka pande zote walipigana katika miji na vitongoji nchi nzima. Mapigano hayo yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 1,000.
Mahakama ya uhalifu wa kimataifa imechukua uwamuzi wa kuhakikisha sheria inatendeka baada ya kuona kuwa juhudi za serikali zinashindwa kuchunguza machafuko yale.

Uchunguzi huo wa kimataifa unaungwa mkono kwa wingi na wananchi wa Kenya. Profesa Maathai aliwalaani walopanga mapigano na alionya kwamba sheria pekee ndiyo itakayowaadhibu walosababisha maafa kwa watu wa Kenya. Maathai alisema uchunguzi unaweza kufika katika kiwango cha juu cha serikali ya Kenya, na aliisii jamii kuunga mkono kazi ya mwendesha mashtaka na kuacha viongozi wao wawajibishwe.

Maathai ataka wakenya waunge mkono ICC
Maathai ataka wakenya waunge mkono ICC

Mjini Kampala jumuia ya kimataifa inapitia maendeleo ya mahakama ya kimataifa tangu kuanzishwa kwake mwaka 2002. Mkutano huo ambao unaanza Jumatatu ijayo utaangalia mkataba wa Rome, ambao unaongoza mahakama hiyo, na namna inavyoweza kukamilisha matakwa yake. Maeneo makuu yanayotarajiwa kuelezewa ni ushirikiano na mahakama za kitaifa na kuwepo kwa mkataba juu ya amani, sheria na waathiriwa wa uhalifu wa kimataifa.

Hatua za Kenya kwenye mkutano yatakuwa moja ya kielelezo cha nia yake ya dhati kuelekea katika sheria kwa waathirika wa ghasia za mwaka 2008. Pia akizungumza katika mkutano, mkurugenzi mkuu wa Africa Centre for Open Governance, Gladwell Otieno, alisema mkutano wa tathmini unawakilisha nafasi ambayo haiwezi kuepukwa na viongozi wa Kenya.

Mkutano wa waandishi wa habari uliandaliwa na Nobel Women’s Initiative, shirika lililoanzishwa mwaka 2006 na wanawake sita washindi wa Tuzo ya Amani akiwemo Maathai, kuimarisha amani duniani, sheria na usawa.
Maathai ni mwanamazingira na mwanaharakati wa kisiasa. Mwaka 2004 alikuwa mwanamke wa kwanza Afrika na raia pekee wa Kenya kushinda Tuzo ya Amani ya Nobel , kwa kazi yake ya kutunza mazingira nchini Kenya.
XS
SM
MD
LG