Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Septemba 17, 2024 Local time: 22:41

Kenya kusaini mkataba wa biashara na Russia


Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov alipokutana na Spika wa Bunge la Kenya, Moses Wetangula huko Nairobi, tarehe 29 Mei 2023. Picha na Kitini / WIZARA YA NJE YA URUSI/AFP.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov alipokutana na Spika wa Bunge la Kenya, Moses Wetangula huko Nairobi, tarehe 29 Mei 2023. Picha na Kitini / WIZARA YA NJE YA URUSI/AFP.

Kenya itatia saini mkataba wa biashara na Russia unaolenga kuimarisha ushirikiano wa kibiashara, ofisi ya Rais William Ruto ilisema siku ya Jumatatu, baada ya kumkaribisha Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Lavrov jijini Nairobi.

Russia imeongeza juhudi zake za kukuza uhusiano wa kiuchumi na bara la Afrika ili kusaidia kukabiliana na uhusiano mbaya uliopo kati ya nchi hiyo na mataifa ya Magharibi, uliochochewa na uvamizi wake nchini Ukraine, inapanga kufanya mkutano wa kilele wa Afrika na Russia huko St Petersburg mwezi Julai.

Ofisiya rais wa Kenya ilisema katika taarifa kwamba biashara baina ya nchi yake na Russia bado iko chini licha ya uwezo uliopo, na mkataba huo utatoa "msukumo unaohitajika" wa kibiashara.

Taarifa hiyo haikusema lini utaratibu wa utiaji saini mkataba huo utakamilika au kutoa maelezo juu ya yale yanayojumuishwa. Kwa sasa Russia inauza zaidi nafaka na mbolea nchini Kenya.

Kuhusu Ukraine, taarifa hiyo ilisisitiza uungaji mkono wa Kenya kuheshimu uadilifu wa kieneo kwa nchi zote, na kuongeza: “Kenya inataka mzozo huo utatuliwe katika msingi unao heshimu pande zote mbili."

Russia imesema uvamizi wake dhidi ya Ukraine, ulioanza tarehe 24, Februari 2022, unalenga kulinda usalama wake dhidi ya Ukraine inayoungwa mkono na uongozi wa Magharibi.

Kyiv na washirika wake wa Magharibi wanaishutumu Moscow kwa kuendesha vita visivyokuwa na uchokozi. Mataifa ya Magharibi yameiwekea vikwazo vya kiuchumi Russia, na kuilazimisha kutafuta uhusiano wa karibu na China, India, na mataifa mengine ya Afrika.

Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la Reuters

Forum

XS
SM
MD
LG