Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Oktoba 07, 2024 Local time: 21:21

Kenya: Hisia mseto baada ya kuahirishwa kwa ufunguzi wa shule hadi 2021


Watoto wa shule nchini Kenya.
Watoto wa shule nchini Kenya.

Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta Jumanne ilifuta kalenda ya masomo ya shule za msingi na upili na vilevile kuahirisha mitihani ya taifa hadi mwaka 2021. 

Waziri wa Elimu nchini humo Professa George Magoha alieleza kuwa kalenda ya masomo 2020 katika shule zote za msingi na upili imefutwa ikimaanisha kuwa wanafunzi wa gredi ya 1 hadi 4, na darasa la tano hadi saba pamoja na kidato cha kwanza hadi cha tatu watasalia katika madarasa hayo mwaka wa 2021.

“Kalenda ya masomo ya mwaka huu itazingatiwa kama ile iliyofutwa kutokana na ueneaji wa virusi vya Corona,” alieleza Prof Magoha.

Bonyeza na kusikiliza:

please wait

No media source currently available

0:00 0:03:36 0:00

Pamekuwa na hofu kuhusu hatma ya mitihani hiyo kufanyika ilivyoratibiwa Novemba mwaka huu kwa watahiniwa wa darasa la nane na kidato cha nne na pia kukamilika kwa mihula miwili iliyobakia.

Kabla kufikia uamuzi huo wizara ya elimu imekuwa ikiendeleza masomo kwa wanafunzi kupitia taasisi ya kuandaa mitaala nchini kwa ushirikiano na shirika la habari la taifa KBC na kupeperushwa kwa vipindi vya masomo kupitia redio, runinga na mtandao. Hata hivyo, changamoto kadhaa zimejitokeza.

Kufuatia utaratibu huo, wanafunzi wa darasa la nane ambao ni watahiniwa wa mtihani wa taifa wa KCPE na wa kidato cha nne ambao ni watahiniwa wa mtihani wa KCSE watatangaziwa ratiba ya mitihani hiyo baadaye mwaka wa 2021.

Lakini japokuwa hatua hii imekuwa ya kushtukiza na yenye lengo la kusaidia serikali kudhibiti maambukizi zaidi ya virusi vya Corona, baadhiya walimu wa shule za kibinafsi na wazazi nchini humo wanaeleza kuwawataathirika pakubwa na hata kudumaa maendeleo ya elimu kwa wanafunzi.

Dan Khasiani Bobea, mwalimu wa shule ya kibinafsi ya Loreto Convent alieleza kuwa uamuzi huo huenda usiwe wenye manufaa kwa walimu.

“Wizara inaposema watoto wasiende shuleni, watoto wanaonekana vijijini, mijini wakiendelea na shughuli zao za kawaida. Watoto hawa wanacheza mpira, wanatazama filamu, wanaenda sokoni, wanatangamana kwingineko. Kwa hivyo linakuwa ni suala la kujiuliza kwamba kwa kweli je, hali ilikuwa mbaya hivyo tusingefungua shule lakini tunaweza kuwaruhusu watoto kufanya haya mambo mengine?”

Washikadau wengine wa sekta ya elimu wanaeleza kuwa pangekuwa na mfumo wa malipo ya mishahara hasa kwa walimu ambao wanalazimika kusubiri zaidi kupata malipo hayo. Erick Kabiduka, ni mwalimu jijini Nairobi.

“Wanaoumia sana ni walimu na wale waliowekeza katika shule za kibinafsi na pia kuna walimu ambao wanafunza shule za serikali lakini wameandikwa chini ya halmashauri. Katika hali hii kuna walimu ambao mwisho walilipwa mshahara mwezi Machi. Maisha ni magumu.”

Kenya iliamuru shule zote vikiwemo vyuo vikuu na taasisi nyingine za mafunzo ya anuai kufungwa Machi 17,2020 wiki tatu kabla ya kukamilika kwa muhula wa kwanza hasa katika shule za upili na msingi.

Jumatatu wiki hii, rais Uhuru Kenyatta ametangaza kuwa usafiri wa ndege wa ndani kwa ndani utarejelewa Julai 15 huku usafiri wa kimataifa ukitarajiwa kuanza Agosti 1, mwaka huu. Vikwazo vingine vya usafiri kutoka jimbo moja hadi jingine vimeondolewa nchini humo.

-Imetayarishwa na Mwandishi wetu wa Nairobi, Kennedy Wandera.

XS
SM
MD
LG