Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 04, 2023 Local time: 05:53

Kenya: Asilimia 52.1 ya Wakenya wanafurahishwa na utendakazi wa rais William Ruto


Rais wa Kenya Dr. William Ruto akihutubia waandishi wa habari, Nairobi, Kenya, Sept. 5, 2022.
Rais wa Kenya Dr. William Ruto akihutubia waandishi wa habari, Nairobi, Kenya, Sept. 5, 2022.

Utafiti ambao umefanywa na shirika la Infotrak, unaonyesha kwamba asilimia 52.1 ya wakenya wanafurahishwa na utendakazi wa rais wa nchi hiyo William Ruto, akiwa amekamilisha siku 100 madarakani tangu alipoapishwa.

Hata hivyo, asilimia 49.2 pekee ya wakenya wanafurahishwa na namna anavyoshughulikia suala la ukuaji wa uchumi wa nchi hiyo yenye uchumi mkubwa Afrika Mashariki.

Utafiti wa Infotrak ulifanyika kati ya Desemba 21 na 22, 2022

Unaonyesha kwamba katika kipindi cha miezi mitatu tangu aingie madarakani, utendakazi wa rais Ruto umekuwa wa chini ikilinganishwa na ahadi alizotoa, bei ya chakula na bidhaa muhimu zikiwa bado ni za juu.

Gharama ya maisha imesalia kuwa juu huku watu wa kipato cha chini wakiendelea kuhangaika zaidi.

Serikali ya Kenya imeondoa ruzuku kwa bidhaa kama unga wa mahindi na mafuta na kupelekea bei ya bidhaa muhimu kuwa ya juu.

Mafanikio ya serikali ya Ruto

Utafiti wa infotrak unaonyesha kwamba hatua ya serikali kurudisha huduma za bandari mjini Mombasa, ni mojawapo ya mafanikio makubwa ya serikali ya Ruto kufikia sasa, ikiwa na asilimia 59.9.

Hatua ya kutenga shilingi bilioni 50 kwa ajili ya vijana kukopa na kuanzisha biashara imetajwa kwenye utafiti huo, ikiwa imeungwa mkono na asilimia 55.8 ya wakenya, ikitajwa kuwa muhimu katika kuwawezesha wakenya wote kujiimarisha kifedha.

Utafiti wa Infotrak unasema kwamba wakenya wanaamini kwamba serikali ya Ruto imefanya vyema katika kuongeza pesa kwa serikali za kaunti ili kuimarisha ukuaji wa uchumi.

Utendakazi wake pia umeungwa mkono na asilimia 57.2 ya wakenya katika uteuzi wa majaji ambao walikuwa wamekataliwa na rais mstaafu Uhuru Kenyatta, kutekeleza mabadiliko katika idhara ya mahakama na polisi.

Zaidi ya nusu ya wakenya wanaunga mkono juhudi zake za kuleta usawa wa kijinsia, asilimia 52.5 ya wakenya wakimuunga mkono uteuzi wa wanawake katika nafasi mbalimbali serikalini.

Mtazamo wa wataalam wa uchumi

Wataalam wa uchumi wameeleza kuwa kazi nzito zaidi inayomkabili Rais Ruto ni kushughulikia madeni mengi, kupunguza mzigo wa mishahara ya sekta ya umma, ukosefu wa ajira, tatizo la chakula na kupunguza gharama ya maisha.

“Hajaangazia sana gharama ya uzalishaji. Amesema kwamba hataangazia ruzuku kwa bidhaa ambayo ilikuwa inawekwa sana na utawala uliopita ili kukabiliana na bei ya mahindi na mafuta. Ikiwa hataweka hii ruzuku, maisha yataendelea kuwa magumu zaidi.

Utafiti wa infotrak pia unaonyesha kwamba wakaazi wa sehemu za mashariki mwa Kenya wanaunga mkono zaidi utendakazi wa serikali kwa zaidi ya asilimia 65.

Malengo ya serikali ya Ruto

Ruwaza ya utekelezaji wa ahadi za rais Ruto imeegemea vigezo tano; kilimo, uchumi wa biashara ndogondogo na za kati, nyumba na makazi, huduma ya afya na mahimizo ya uchumi kidigitali na ubunifu.

Wanasiasa wa upinzani wakiongozwa na Raila Odinga, wamekuwa wakikosoa serikali ya Ruto kwa kile wamedai kama kushindwa kutekeleza ahadi alizotoa, wakisisitiza kwamba ilikuwa makosa kuondoa ruzuku kwa mafuta na unga.

Rais Ruto amesema kwamba ruzuku sio suluhisho la kupanda kwa gharama ya maisha na kwamba linalohitajika ni kuimarisha uzalishaji, hasa wa chakula, akisisitiza kwamba wapinzani wake wanastahili kumpa muda kutekeleza ahadi alizotoa.

Imetayarishwa na Kennedy Wandera, VOA, Nairobi

XS
SM
MD
LG