Viongozi wa Kenya waliapa Jumapili kwamba watawasaka waasi wa kundi la Al-Shabaab kutoka Somalia kufuatia miripuko miwili iliyosababisha kifo cha mtu mmoja na watu 31 kujeruhiwa katika mji wa pwani wa Mombasa, lakini hawakuwalaumu moja kwa moja kundi hilo wakidai uchunguzi unaendelea.
Miripuko hiyo iliyotokea karibu wakati mmoja ilitokana na grunetti lililorushwa kwenye mkusanyiko wa kidini katika mtaa wa Mtwapa kaskazini mwa Mombasa na bomu lililotengenezwa kiyenyeji lililotupwa kwenye mgahawa mtaani Tononoka karibu na uwanja mkuu wa michezo wa Mombasa.
Kundi la Al-Shabaab lenye uhusiano na Al-Qaeda limeshafanya mashambulizi nchini Kenya tangu serikali kupeleka wanajeshi wake Somalia mwezi Oktoba mwa uliyopita kuwasaka wanaharakati hao.
Hata hivyo shambulio la Jumamosi ni la kwanza kutokea Mombasa, moja wapo ya kituo kikuu cha utali nchini humo na limetokea wiki moja kabla ya kuanza majira ya utali mnamo siku kuu ya Pasaka.
Waziri wa usalama wa ndani George Saitoti amewambia waandishi habari mjini Mombasa kwamba , “hatutachoka kamwe kuwatafuta watu hawa hadi tumewamaliza. Wananchi wetu lazima wapate usalama. Hatuwezi kukubali watu kutoka sehemu nyingine waloharibu nchi yao halafu wanakuja kuharibu taifa hili.”
Waziri mkuu Raila Odinga akifuatana na Saitoti alijaribu kuwahakikishia watali usalama wao baada ya miripuko hiyo.
“Kenya ni nchi Salama, mtu asiwatishiye watali. Watali waendele kwenda Kenya.”
Wanajeshi wa kenya walipelekwa kusini mwa Somalia baada ya mashambulio mawili tofauti dhidi ya miji ya mapumziko kaskazini mashariki ya nchi hiyo.
Shambulio la Jumamosi limezusha hofu kwamba biashara ya utali moja wapo ya biashara tatu kuu inayoipatia nchi hiyo fedha za kigeni huwenda ikaathirika kwa watali kuahirisha safari zao wakati huu wa pasaka.
Idara za usalama za kenya zimaanza uchunguzi kujuwa walohusika na mashambulio hayo yaliyosababisha kifo cha mtu mmoja.
Hadi hivi sasa mashambulio yamekua yakitokea Nairobi na miji ya kaskazini mashariki karibu na mpaka wa Somalia.