Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Mei 02, 2024 Local time: 01:06

Kashfa mpya ya ufisadi yaibuka Kenya


Wakenya waandamana kwenye barabara za Naairobi kupinga ulaji rushwa katika idara za serikali na mashirika ya umma.
Wakenya waandamana kwenye barabara za Naairobi kupinga ulaji rushwa katika idara za serikali na mashirika ya umma.

Sakata nyingine ya ufisadi inayokumba utawala wa Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, imejitokeza baada ya tume iliyochunguza jinsi pesa za umma zilivyotumiwa na idara ya misitu, kutoa ripoti inayoonyesha kwamba takriban shilingi bilioni mbili, zilizotengewa  mradi wa upandajji miti katika shule kwenye maeneo mbalimbali ya nchi, zimepotea.

Pesa hizo zilikuwa zimetolewa na serikali ili kufadhili utoaji wa mafunzo kwa watoto wa shule, kuhusu upandaji miti, kuanzisha bustani za miche katika shule za umma kote nchini, na kufadhili kampeni ya kitaifa iliyonuiwa kuhakikisha kwamba asili mia 10 ya ardhi yote inayokaliwa na shule za umma, imejaa miti.

Waziri wa mazingira na misitu nchini Kenya, Keriako Tobiko, alisema Jumapili kwamba aliwasilisha ripoti hiyo, pamoja na majina ya washukiwa wa sakata hiyo, kwa tume ya maadili na kupambana na usfisadi, (EACC), na ripoti nyingine kando yake ikapelekwa kwa mhasibu mkuu wa serikali.

Ripoti hiyo inadai kwamba maafisa wa ngazi za juu serikalini waligeuka na kuwa wafanya biashara haramu wa kuuza mbao na kutumia akaunti binafsi kukusanya ushuruu wa serikali.

Sikiliza:

please wait

No media source currently available

0:00 0:03:09 0:00

Iwapo madai hayo yatathibitishwa kuwa ya kweli, basi huo utakuwa mradi wa upandaji miti wenye gharama kubwa Zaidi katika historia ya nchi hiyo.

Haya yanajiri huku serikali ya Kenya ikikabiliwa na kashfa nyingine kadhaa za ufisadi, ikiwa ni pamoja na ile ya taasisi ya taifa ya huduma ya vijana, NYS, ambako takriban shilingi bilioni tisa zinadaiwa kufujwa, na ile ya bodi ya kitaifa ya nafaka na mazao, NCPB, ambayo imepelekea baadhi ya Wakenya kuishutumu serikali ya Kenyatta kwa kile wanachokiita "usimamizi mbaya wa mashirika ya serikali."

Utawala wa Kenyatta hata hivyo, umesema kuwa watakaopatikana na hatia ya kufuja fedha za umma, watavchukuliwa hatua kali. Naibu wa rais William Ruto amesema kuwa angetaka kuona washukiwa wakifunguliwa mashtaka.

"Safari hii hawataepuka. Hatuwezi kuwa tunasema jambo lile lile miaka nenda miaka rudi," Ruto alisema katika hotuba akliyoitoa Jumamosi.

Tayari Rais Kenyatta amepokea barua za kujiondoa kwa Katibu mkuu wa wizara hiyo ya Vijana, Lilian Omollo, na Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo ya NYS Richard Ndubai ili kutoa nafasi ya uchunguzi kufanyika.

Wiki iliyopita, Waziri wa Utumishi kwa Umma, Vijana na Jinsia Margaret Kobia, alifika mbele ya kamati ya bunge la kitaifa ya leba na kuelezea anayoyafahamu kutokana na kashfa hii na kusisitiza kuwa uchunguzi umekuwa ukiendelea na hivyo kuhitaji muda zaidi kwa uchunguzi kubaini kilichojiri.

Hata hivyo, Wakenya katika maeneo mbalimbali ya nchi hawajaridhika na ahadi za serikali kwamba iytachukua hatua, na wanaeleza kwamba wamsikia ahadi kama hizo miaka nenda miaka rudi.

Hii si mara ya kwanza fedha za umma zimefujwa katika taasisi ya NYS, Mwaka 2016, zaidi ya shilingi bilioni 1.8 ziliripotiwa kufujwa huku aliyekuwa waziri wa Ugatuzi wakati huo Anne Waiguru ambaye sasa ni gavana wa jimbo la Kirinyaga akilazimika kujiuzulu na wengine waliotajwa katika sakata hiyo wakiachiliwa kwa dhamana na mahakama.

Wachambuzi wanasema kuwa safari hii, huenda rais Kenyatta akaonyesha ujasiri usio wa kawaida katika kupambana na ufisadi, tofauti na alivyolishughulikia janga hilo katika siku za nyuma.

-Mwandishi wa VOA, Kennedy Wandera alichangia ripoti hii.

XS
SM
MD
LG