Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Mei 28, 2023 Local time: 19:49

Kampeni kali yazinduliwa dhidi ya Al-Shabab


Vifaru vya AMISOM katika shughuli zake za kijeshi dhidi ya kundi la Al-Shabab nchini Somalia

Kikosi cha AMISOM kimezindua kampeni katika wilaya ya Daynile na magharibi ya Mogadishu dhidi ya wanamgambo wa kundi la Al-Shabab

Vikosi vya Somalia kwa kuungwa mkono na majeshi ya Umoja wa Afrika yamezindua kampeni kali ya kutimua wanamgambo wa al-Shabab katika vitongoji vya Mogadishu hususan kwenye ukanda wa Afgoye.

Maafisa wa ulinzi wanasema lengo la kampeni hiyo ni kuleta uthabiti na amani kwa watu 400,000 waliofurushwa makwao katika eneo la Afgoye lililoko magharibi ya mji wa Mogadishu. Hii ni mara ya kwanza vikosi vya Umoja wa Afrika na majeshi ya kitaifa ya Somalia kuungana pamoja kushambulia vituo vya wanamgambo wa al-Shabab nje ya Mogadishu.

Msemaji wa kikosi cha Umoja wa Afrika kinachojulikana kama AMISOM- Paddy Ankunda, aliiambia Sauti ya Amerika kuwa kampeni dhidi ya al-Shabab ilizinduliwa katika wilaya ya Daynile na kuelekea magharibi mwa Mogadishu kuingia katika eneo la Afgoye.

Alisema wilaya ya Daynile sasa imo mikononi mwa majeshi ya AMISOM na kwamba wanapigania kijiji kidogo kiitwacho Elasha Biyaha kilichoko karibu na Afgoye na ripoti za hivi karibuni alizopata ni kwamba majeshi ya Umoja wa Afrika sasa yanadhibiti asilimia 85 ya kijiji hicho.

Eneo la Afgoye lina watu 400,000 waliofurushwa makwao kwenye eneo la kilomita 30 mraba kutoka mji mkuu wa Mogadishu. Ni mahala ambapo watu wengi kutoka Mogadishu wamepiga kambi katika kipindi cha mwaka mmoja baada ya mji huo mkuu kushambuliwa kwa risasi kila siku katika mapigano baina ya vikosi vya serikali na wanamgambo wa al-Shabab.

Mashirika ya kutoa misaada ya kibinadamu yameeleza wasiwasi wao juu ya raia wanaojeruhiwa katika mtafaruku huo na kuziomba pande zote kuepuka kutumia nguvu na kupigana kiholela ambapo raia wanajikuta wamenaswa kwenye mapigano hayo.

Vikosi vya Umoja wa Afrika vilifanikiwa kiasi kikubwa kutimua wanamgambo hao wa Kiislam mwaka jana mjini Mogadishu na kuimarisha kwa kiwango kikubwa mji huo mkuu. Lakini eneo la Afgoye ni mojawapo ya maeneo yaliyobaki mikononi mwa wanamgambo wa al-Shabab.

Wanamgambo hao walilifanya eneo hilo kuwa ngome yao ambapo walikuwa wakiwaandikisha wanachama wapya na hata kuwapa mafunzo na pia kulifanya eneo kuwa la mkutano wa viongozi wake ambapo wanaeneza propaganda zao.

XS
SM
MD
LG