Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Julai 27, 2024 Local time: 04:28

Kilichomfanya kamishna wa IEBC Roselyn Akombe ajiuzulu


Aliyekuwa kamishna wa tume ya uchaguzi na mipaka ya Kenya, Dkt Roseline Akombe Kwamboka.
Aliyekuwa kamishna wa tume ya uchaguzi na mipaka ya Kenya, Dkt Roseline Akombe Kwamboka.

Mmoja wa makamishna wa tume ya uchaguzi na mipaka ya Kenya, IEBC, alijiuzulu Jumatano, siku nane tu kabla ya zoezi la marudio la kumchagua rais lililopangwa kufanyika Alhamisi wiki ijayo.

Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, Kamishna Roselyne Akombe Kwamboka alisema alijiuzulu kwa sababu tume hiyo "imeingiliwa kisiasa na kutumbukia kwenye mzozo unaoendelea kuikumba nchi ya Kenya."

Akombe, ambaye alituma taarifa hiyo akiwa mjini New York, Marekani, aidha alieleza kwamba amekuwa akitathmini suala la kujiuzulu kwa muda mrefu.

"Lakini nimevumilia kwa matumaini kwamba, kwa pamoja, tungepata njia za kutatua mzozo unaotukabili kama taifa," alisema Akombe.

Kamishna huyo wa zamani alisema kuwa imekuwa vigumu kwake kwendelea kuhudhuria mikutano ya tume hiyo huku makamishna wenzake wakionekana kuwa tayari kupiga kura kwa misingi ya kuegemea.

"Imekuwa vigumu mno kwangu kwendelea kuonekana kwenye vituo vya telkevisheni nikitetea misimamo ya tume hiyo ambayo binafsi sikubaliani nayo. Ni dhahiri kwamba mchango wangu kwa IEBC na taifa kwa jumla ni mdogo mno," alieleza.

Akombe alisema kuwa kwa maoni yake, tume hiyo haiko tayari kusimamia uchaguzi wa haki na wa kweli.

Alisema bado kuna muda wa kuiokoa nchi kutoka kwa mzozo unaoikabili.

"Inahitaji tu watu wachache wenye uadilifu kusimama na kusema kuwa hatuwezi kwendelea na uchaguzi wa tarehe 26 mwezi huu kama ulivyopangwa," alisema.

Dkt Akombe alisema anasikitika kwamba baadhi ya maafisa wa tume hiyo wamekuwa wakikabiliwa na hali ya utovu wa usalama na tishio kwa maisha yao.

Na akizungumza na kituo cha televisheni cha KTN kwa njia ya simu siku ya Jumatano, Akombe alikariri aliyosema kwa kimoja cha vituo vya habari vya kimataifa kuwa ana hofu kwamba maisha yake yalikuwa hatarini lakini hakufafanua kauli hiyo.

Je Roslyn Akombe ni Nani?

Akombe alikuwa mmoja wa makamishna saba wa tume ya IEBC.

Kabla ya kujiunga na tume hiyo, Akombe alifanya kazi kama afisa mwandamizi wa umoja wa mataifa mjini New York.

Aliiambia kamati iliyomfanyia mahojiano kabla ya kuajiriwa kama kamishna kwamba alikuwa na tajriba kubwa ya kidiplomasia baada ya kuishi nje ya nchi kwa miaka 15.

Akombe, mwenye umri wa miaka 41, alikuwa amechukua likizo ya bila malipo kutoka kwa kazi yake ya naibu wa katibu kwenye umoja wa mataifa.

Mahakama ya juu nchini Kenya ilibatilisha matokeo ya uchaguzi uliofanyika tarehe nane mwezi Agosti na kuamuru kuwa uchaguzi wa marudio ufanyike kwenye kipindi cha siku sitini kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo.

Hali ya vuta nikuvute iliibuka huku muungano wa upinzani, NASA, ukiongozwa na aliyekuwa mgombea wake Raila Odinga, ukishikilia kwamba uchaguzi huo hauwezi kufanyika kabla ya mageuzi kufanywa kwenye tume ya IEBC na mchakato mzima wa uchaguzi huo.

IEBC imekuwa ikishikilia kwamba imefanya baadhi ya mabadiliko na kwamba uchaguzi utafanyika kama ilivyopangwa. Chama kinachotawala cha Jubilee kikiongozwa na rais Uhuru Kenya kimeshikilia msimamo huo huo na kimekuwa kikiendelea na kampeni za kuwarai wafuasi wake kujitokeza kwa wingi ili kumpigia kura mgombea wake.

Mgombea kwa tikiti ya muungano wa NASA, alitangaza kwamba hatashiriki kwenye uchaguzi wa tarehe 26.

Imeandikwa na BMJ Muriithi akiwa Nairobi, Kenya.

XS
SM
MD
LG