Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Septemba 22, 2023 Local time: 18:49

Mahakama Kenya Yaamua Kambi ya Dadaab Iendelee Kuhudumia Wakimbizi


Wakimbizi wakiwa katika kambi ya Ifo huko Dadaab, karibu na mpaka wa Kenya na Somalia.

Mahakama kuu Kenya imeitaka Serikali kutofunga kambi ya wakimbizi ya Dadaab, ikisema kuwa uamuzi huo ni kinyume cha Katiba.

Wasiwasi juu ya kufungwa kwa kambi ulikuwa ukiendelea tangu Mei 2016, wakati serikali ilipotangaza itawarudisha wakimbizi wa kisomali nchini kwao ifikapo mwisho wa Novemba 2016 na kuivunja Idara ya Masuala ya Wakimbizi. Kenya imesema hatua hiyo ilitokana na tishio la usalama.

Jaji wa mahakama kuu, JM Mativo alitoa uamuzi Alhamisi kwamba amri zilizotolewa na serikali zilikuwa za kibaguzi na adhabu ya pamoja kwa wakimbizi.

Dadaab ni kambi kubwa ya wakimbizi kuliko zote ulimwenguni, inayotoa hifadhi kwa takriban wakimbizi 300,000, wengi wao ni Wasomali.

Mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili VOA aliongea na wakimbizi ambao wameeleza kufurahishwa na uamuzi huo wa mahakama.

"Huo uamuzi nimeupokea vizuri, lakini huko nyuma walipokuwa wametoa uamuzi wa kufunga kambi hawakufanya vizuri kwani wakimbizi wangeenda wapi wakati huko Somalia hakuna amani," alisema kijana mmoja kwenye kambi hiyo.

Pia mkimbizi mwingine ameiambia VOA kuwa "Somalia hakuna amani na ndio maana tumebakia hapa kwenye kambi ya Daadab, sio kwa sababu ya chakula. Somalia ikirudi kuwa salama Wasomali wataondoka Daadab kurudi kwao."

Kupingwa kwa maamuzi ya serikali kufunga kambi ya Dadaab na kuivunja Idara ya Masuala ya Wakimbizi kumekuja katika ombi lililotolewa na taasisi mbili za haki za binadamu Kenya.

Serikali ya Kenya haijajibu mara moja juu ya uamuzi wa mahakama.

Shirika la Amnesty International limepongeza uamuzi wa mahakama, likisema kuwa “inaonyesha wajibu wa Kenya kikatiba na kwa sheria za kimataifa” katika kuwalinda wale wanaotafuta hifadhi kutokana na maisha yao kuwa hatarini.

Shirika la Human Rights Watch limesema mahakama imetuma ujumbe kuwa ni taasisi moja tu Kenya ambayo ina haki ya kulinda haki za wakimbizi.

“Baada ya miezi mingi ya wasiwasi kuhusu kufungwa kwa kambi na tarehe za mwisho za utekelezaji wake ukiumiza vichwa vyao, pamoja na kuongezeka kwa masharti ya kuomba hifadhi na utawala wa Marekani hivi karibuni ukisimamisha kwa muda kuruhusu wakimbizi kuingia nchini, uamuzi wa mahakama umetoa faraja kwa wakimbizi wa kisomali,” mtafiti wa HRW Afrika Laetitia Bader amesema.

Na kuongezea kwamba hivi sasa wakimbizi hao wana matumaini kwamba wana maamuzi mbali ya kurejea Somalia ambayo imegubikwa na hali ya ukosefu wa usalama na ukame.

XS
SM
MD
LG