Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 19, 2024 Local time: 23:36

Kagame: Monusco wanajua kuhusu waasi wa FDLR kuwa ndani ya jeshi la DRC


Rais wa Rwanda Paul Kagame akihutubia wanajeshi wa nchi hiyo baada ya mafunzo
Rais wa Rwanda Paul Kagame akihutubia wanajeshi wa nchi hiyo baada ya mafunzo

Rais wa Rwanda Paul Kagame amesema kwamba amejiandaa kwa mabaya wakati uhusiano kati ya nchi yake na Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo ukiendelea kuharibika, lakini anaitakia Congo mazuri namna anavyoitakia Rwanda.

Ameshutumu jeshi la umoja wa mataifa Monusco, akidai kwamba limekuwa likijua kwamba jeshi la Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo limekuwa likishirikiana na waasi wa Democratic forces for liberation of Rwanda FDLR, lakini likaamua kunyamaza.

Kagame ameshutumu serikali ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo kwa “kuunga mkono” wapiganaji wa kundi la Democratic forces for the liberation of Rwanda - FDLR, wanaoshutumiwa kwa kusababisha mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda.

Katika mahojiano na televishineni ya serikali ya Rwanda RTV, Kagame amedai kwamba jeshi la umoja wa mataifa MONUSCO, “linajua kwamba DRC inawasaidia wapiganaji wa FDLR”.

Monusco wameshirikiana na jeshi la serikali na kundi la waasi?

Rais huyo wa Rwanda amedai kwamba jeshi la Congo, linasaidiwa na wapiganaji wa FDLR kupigana na waasi wa M23.

“Wapiganaji wa FDLR wamekuwa wakishirikiana na jeshi la Congo kupigana na kundi la M23, Umoja wa mataifa nao ulijihusisha wakisema wanasaidia jeshi la Congo lakini walijua jeshila serikali lilikuwa linashirikiana na kundi la FDLR dhidi ya M23. Kundi la M23 lilikuwa linapambana na Monusco, jeshi la serikali na waasi wa FDLR. Kundi la FDLR lilistahili kuwa limepigwa, kumalizwa nguvu na kurudishwa nyumbani.” Amesema Kagame akiongezea kwamba “hayo ndio yamekuwa yakifanyika. wamekuwa wakirusha makombora ndani ya Rwanda, kuharibu mali na kusababisha vifo. Wamefanya hivyo mara kadhaa.”

Shutuma za Congo dhidi ya Rwanda

Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo imekuwa ikishitumu Rwanda kwa kuunga mkono waasi wa M23, huku Rwanda ikiishutumu DRC kwa kuunga mkono wapiganaji wa FDLR.

Kagame amesema kwamba “haiwezi kukubalika kwamba kundi la FDLR linaweza kuvuka mpaka na kuingua nchini mwetu au hata kurusha makombora ndani ya mipaka yetu na kuuwa watu wetu. Hatujafanyia hilo Congo.”

Akiwa Congo Brazzaville, mwamnzoni mwa mwezi Juni, Rais wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi alisema kwamba hana “shaka yoyote kwamba Rwanda inaunga mkono waasi wa M23 kushambulia serikali yake.”

Kagame amjibu Tshisekedi

Kagame amemjibu Tshisekedi akisema “nashindwa kuelewa kwa nini rais wa Congo alisema kitu kama hicho. Anastahili kujua vizuri kwamba ukweli upo. Tumezungumzia haya mambo mara nyingi tangu alipoingia madarakani na kabla ya mgogoro huu kuanza.”

Waasi wa M23 wamedhibithi mpaka wa Bunagana baada ya kuua kamanda wa jeshi la Congo na kupelekea wanajeshi wa Congo kukimbilia Uganda.

Mapigano ya M23 na majibizano kati ya Rwanda na DRC yamepelekea kuongezeka kwa ujumbe wa chuki katika eneo lote la Kivu kaskaini zinzoelekezwa dhidi ya watu kutoka jamii ya Watutsi.

“DRC wamekuwa na tabia kama ya Watoto walioharibika. Wanajisababishia matatizo halafu wanaanza kulia na kupaaza sauti wakisema kwamba kuna mtu anawachokoza.” Amesema rais wa Rwanda Paul Kagame akiongezea kwamba “bahati mbaya kuna mataifa katika baadhi ya sehemu za dunia yanayounga mkono DRC hata kama ndio wenye makosa. Hili lilikuwa swala kubwa katika miaka iliyopita. Tulieleza lakini hakuna aliyetaka kutusikiliza. Mara hii walifanya makosa maksudi ambayo kila mtu aliona. Walianzisha vita ambavyo havikuwa na msingi wowote.”

Raia wa Congo wanaozungumza Kinyarwanda wanastahili kusikilizwa

Rais huyo wa Rwanda amesema kwamba kuna haja kubwa ya kutatua matatizo ya raia wa Congo wanaozungumza Kinyarwanda, wakiwemo waasi wa M23.

“Hiyo ni shida ya Congo kutatua, sio yangu.” Amesisitiza Kagame.

“Wanazungumza Kinyarwana lakini ni raia wa Congo. Namna walivyojipata kuwa raia wa Congo haiwezi kuwa lawama kwa Rwanda au Congo. Unawezaje kuamua kwamba watu hao sio raia wa nchi yao? Unaanzia wapi? Hata utawezaje kufanikisha hilo?” ameuliza Kagame.

“Natakia Congo mema. Lakini mema yasipokuja, watanipata kama nimejitayarisha kwa mabaya Zaidi. Najitayarisha kwa mabaya lakini nawatakia mema.Namaanisha ninachosema. Natakia Congo mema, na natakia mema nchi yangu ya Rwanda.”

Kagame aitisha mazungumzo

Rais huyo wa Rwanda amesisitiza kwamba mgogoro wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo unaweza kusuluhishwa tu kwa kupitia kwa mazungumzo na wala sio kwa vita.

Kagame na mwenzake wa Congo Felix Tshisekedi, wamepangiwa kukutana nchini Angola hiileo Jumatano kwa mazungumzo yatakasimamiwa na rais Joao Lourenco.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG