Michael Jordan, ambaye ni mmoja wa wachezaji wa zamani wanaofahamika ulimwenguni kote kwa ustadi wa kucheza mchezo wa Kikapu, amevunja kimya chake na kusema kuwa amekuwa akisikitishwa mno na visa vya kuuawa kwa Wamarekani weusi, vinavyotekelezwa na polisi.
Katika ujumbe kwa njia ya barua ya ukurasa mmoja iliyochapishwa na mtandao wa undefeated.com, ambao unamilikiwa na shirika la utangazaji la ESPN leo Jumatatu, Jordan, ambaye pia ni mmiliki wa klabu cha NBA cha Charlotte Hornet, alisema kuwa hawezi kuendelea kunyamaza kuhusiana na swala hilo.
Aidha Jordan ametangaza kupita barua hiyo, kwamba atatoa msaada wa dola milioni mbili - milioni moja ikienda kwa taasisi mpya ya uhusiano wa polisi na raia, iliyoundwa na chama cha kimataifa cha wakuu wa polisi, na milioni moja ikienda kwa idara ya kisheria ya chama cha masilahi ya watu wasio wa rangi nyeupe, NAACP.
Kwa mujibu wa mtandao huo wa undefeated.com, Jordan pia alielezea kutoridhika kwake na mashambulizi yanayowalenga maafisa wa kulinda usalama. Mchezaji huyo wa zamani alisema kuwa kama mtu mweusi ambaye anajivunia kuwa Mmarekani, na kama mtu ambaye alipoteza baba yake kupitia kupigwa risasi na majambazi mnamo mwaka wa 1993, amekuwa akihuzunishwa sana na visa hivyo.
Kituo cha televisheni cha CNN kiliripoti Jumatatu kuwa licha ya Jordan kuwa na ushawishi kutokana na umaarufu wake, kabla ya kutoa tangazo hilo, alikuwa mchache wa maneno kuhusiana na maswala yanayokumba jamii ya Wmarekani, jambo ambalo limepelekea baadhi ya wenzake kumkosoa.
Barua hiyo ya Jordan ilijiri takriban wiki mbili na nusu baada ya mwanajeshi wa zamani kuwapiga risasi na kuwaua maafisa watano wa polisi mjini Dallas, jimbo laTexas, huku akisema kuwa alikuwa na hasira kwa sababu ya polisi kuwawapiga risasi na kuwaua Wamarekani weusi.
Katika siku za hivi karibuni, swala la mauaji ya watu weusi na lile la kuuawa kwa maafisa wa polisi kwa kupigwa risasi na Wamarekani weusi limezua hisia mbali mbali huku baadhi ya wananchi wakiandamana kuelezea kutoridhika kwao.