Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Desemba 07, 2022 Local time: 19:20

Jinsi wanasiasa wanavyopigania kura za vijana katika uchaguzi mkuu


Mgombea kiti cha Rais Patrick Amuriat Oboi akifanya campani miongoni mia vijana

Uganda inajitayarisha kwa uchaguzi mkuu Januari 14 2021. Rais Yoweri Museveni anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa wagombea wengine 10.

Museveni mwenye umri wa miaka 76 anagombea mhula wa sita madarakani. Anakabiliwa na ushindani kutoka kwa wagombea wengine ambao baadhi yao ni vijana, akiwemo John Katumba mwenye umri wa miaka 24.

Wagombea wengine ni Nancy Kalembe (34) ambaye ndiye mgombea pekee wa kike, Willy Mayambala (35), Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine (38), Joseph Kabuleta Kiiza (48), Nobert Mao (53), Patrick Amuriat Oboi (57), aliyekuwa waziri wa usalama Lt. Gen. Henry Tumukunde (61), aliyekuwa kamanda wa jeshi Generali Mugisha Muntu (62) na Fred Mwesigye (64).

Idadi ya vijana waliosajiliwa kupiga kura

Kulingana na tume ya uchaguzi ya Uganda jumla ya watu 17,658,527 wameandikishwa kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2021.

Asilimia 76 kati ya hao ni vijana wenye umri kati ya miaka 18 na 35, ikiwa na maana kwamba kura za vijana zinatosha kuamua uongozi wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Wachambuzi wanasema idadi ya vijana watakaojitokeza kupiga kura nido itaamua mstakabali wa taifa hilo.

Vijana wakishiriki katika kampeni za Mgombea wa urais Yoweri Museveni nchini Uganda
Vijana wakishiriki katika kampeni za Mgombea wa urais Yoweri Museveni nchini Uganda

Mchambuzi Crispin Kaheru wa muungano wa kufuatilia demokrasia nchini Uganda CEDU, amesema kwamba idadi ya vijana ambao wanagombea viti mbalimbali katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2021 imeongezeka zaidi ikilinganishwa na ilivyokuwa katika uchaguzi wa mwaka 2011 na 2016.

Amesema kwamba idadi ya wagombea wa viti vya bunge wenye umri kati ya miaka 18 na 35 imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 30 ikilinganishwa na uchaguzi wa mwaka 2016.

“Ni wazi kwamba ujumbe wa wagombea wengi unaangazia sana maslahi ya vijana na namna ya kuimarish maisha yao na kuifanya Uganda kuwa nchi ambayo imeendelea katika kila sekta.” Amesema Kaheru.

Ukosefu wa ajira kwa vijana

Chini ya asilimia 15 ya vijana wameajiriwa na wana kipato cha kutegemewa kila mwezi.

Waziri wa leba, jinsia na maendeleo ya mijini Frank Tumwebaze katika mojawapo ya vikao na waandishi wa habari kwenye kituo cha habari cha serikali, amesema kwamba hakuna shaka kwamba vijana wengi wamejiingiza katika siasa na kwamba hii itabadilisha siasa za nchi hiyo kwa namna moja ama nyingine au namna kampeni zinavyofanyika au ujumbe katika kampeni.

“Jambo zuri ni kwamba idadikubwa ya vijana nchini Uganda wana elimu ya kutosha na wanaweza kufanya maamuzi sahihi bila kudanganywa na mtu yeyote.” Alisema Tumwebaze akiongezea kwamba “ni werevu sana kutambua mgombea anayetoa ahadi za uongo na yule mwenye rekodi yakuaminika. Hakuna kwa hawa wagombea wote, mwenye ujuzi wa uongozi kumshinda rais Yoweri Museveni.”

Tumwebaze, mwenye umri wa miaka 45, anadai kwamba kuwa kijana sio kibali tosha cha kuambia mtu kwamba “mimi ni kijana, nipigie kura. Ni zaidi ya umri wako. Inahusu namna unavyozungumza na wapiga kura. Kile unachoweza kufanya na kujenga hali nzuri ya baadaye kwa raia wa nchi hii. Kumkosoa rais Museveni kila mara haitoshi kukuingiza madarakani.”

Vijana wakiwa katika kampeni za Bobi Wine nchini Uganda
Vijana wakiwa katika kampeni za Bobi Wine nchini Uganda

Mbinu zinazotumika kutafuta kura za vijana

Tume ya uchaguzi imetaka wagombea wote kufanya kampeni ambayo imetajwa kuwa ya kisayansi kutokana na janga la virusi vya Corona.

Rais Yoweri Museveni amesisitiza kwamba hakuna mgombea anayestahili kuruhusiwa kuhutubia umati mkubwa wa watu, na polisi wamekabiliana na wafuasi wa wagombea wa upinzani hasa wa Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine na wa chama cha Forum for democratic change -FDC, Patrick Amuriat Oboi.

Wengi wa wafuasi wa upinzani ni vijana.

Wagombea wengine wa viti mbali mbali wa chama cha Museveni NRM, hata hivyo, wamekuwa wakihutubia umati mkubwa wa watu bila kutawanywa na polisi.

Ili kuwafikia vijana wagombea wote wanaendelea kutumia mitandao ya kijamii hasa facebook na twiter.

Museveni, licha ya miaka iliyopita kusema kwamba mitandao ya kijamii ni ya kueneza udaku, amekumbatia sana facebook na twiter, na naitumia kufanya kampeni yake kila siku.

Hivi karibuni, Museveni alizindua App kwa jina ‘Mzee NALO’ maana yake kwamba ‘Tunamuunga mkono mzee Museveni’.

App hiyo ni mojawapo ya mbinu anazotumia kuwafikia vijana anapotafuta kura zao. Inaonyesha mafanikio yote ya Museveni ya miaka 34 ambayo amekuwa madarakani, na miradi ambayo anataka kutekeleza katika miaka 5 ijayo.

Mzee NALO app ni mbinu ya hivi punde ya rais Museveni kutafuta kura za vijana na kuongeza ushindani dhidi ya Katumba (24) Kalembe (34) Mayambala (35) Kyagulanyi (38) na Mesigye (39) ambao wanavutia sana kura za vijana.

Vijana wakiwa katika kampeni ya mgombea urais John Katumba nchini Uganda.
Vijana wakiwa katika kampeni ya mgombea urais John Katumba nchini Uganda.

Museveni pia anatumia #M7 Bazzukulu kuwafikia vijana ambao mara nyingi anapozungumza nao kupitia mitandao hiyo ya kijamii, huwa anasema anawapenda namna babu anavyowapenda wajukuu wake. Bazukulu ni neno la kiganda linalomaanika wajukuu.

Bobi Wine anatumia sana ukurasa wake wa facebook kuwafikia vijana. Kando na ukurasa wake binafsi, anatumia pia ukurasa wa Ghetho TV kuonyesha moja kwa moja mikutano yake ya kampeni kote Uganda, na ana wafuasi wengi.

Ili kuwavutia vijana zaidi, anatumia nyimbo zake kuwatumbuiza kabla ya kuwahutubia.

Ili kukabiliana na mbinu hii, Museveni naye anatumia ukurasa wake wa facebook kuonyesha mikutano yake ya kampeni moja kwa moja kila alipo. Anatumia pia mwanamuziki Moses Saali, maarufu Bebe Cool kuwavutia vijana kwa kambi yake.

Mbinu hii pia inatumika na wagombea wengine wote wa urais na imefikia kiwango ambacho Museveni na Bobi Wine wanahutubia wafuasi wao wakati mmoja katika kupinga nguvu ya nani aliye na wafuasi wengi kwenye mitandao ya kijamii.

Kuwapa vijana nafasi na kuimarisha mapato yao

Mgombea wa urais kwa chama cha Democratic Nobert Mao, amekuwa akisisitiza kwamba lengo lake kuu ni kuweka mazingira ya kutoa fursa kwa vijana kujiimarisha kimapato.

Alitoa fursa kwa vijana wasiozidi umri wa miaka 30 ambao aliwaita kama UB30, kuzindua picha ya kampeni yake na kuwalipa walioshiriki na kufanya kazi bora zaidi.

UB30 ni ujumbe wa kuwavutia vijana wanaopenda muziki wa kundi la wanamuziki UB40.

Kyagulanyi ametoa fursa kwa vijana kugombea viti mbalimbali katika chama chake cha NUP.

Wagombea maarufu ambao wamekuwa wanasiasa kwa mda mrefu nchini Uganda walinyimwa tiketi ya chama cha Bobi Wine, na kupewa vijana ambao wengi wao hawakuwa na umaarufu wowote.

“Nchi yetu inakumbana na hali mbaya ya ukosefu wa ajira na serikali yetu inazingatia namna ya kubuni nafasi za kazi na kuweka mazingira mazuri ya biashara, kupunguza gharama ya umeme, riba kwa mikopo na kupambana na ufisadi.” Alisema Kyagulanyi katika hotuba yake baada ya kuidhinishwa na tume ya uchaguzi kugombea urais.

Je, vijana watajitokeza kupiga kura?

Wachambuzi wanasema kwamba wagombea wote wanajaribu uwezo wao wote kuwavutia vijana kuwaunga mkono kwa kutumia kila mbinu, lakini kila mmoja ana changamoto zake.

Vijana wakiwa katika kampeni za mgombea urais John Katumba nchini Uganda.
Vijana wakiwa katika kampeni za mgombea urais John Katumba nchini Uganda.

“Rais Museveni anatumia ujumbe wa kuzindua miradi inayoleta utajiri wakati anafahamu vyema kwamba vijana wengi ambao wamezaliwa akiwa madarakani wanapitia hali ngumu ya kiuchumi. Kwa upande mwingine mshindani wake anayeonekana kumsukuma sana ambaye ni Bobi Wine, anaonekana kutumia ujumbe kwamba ni kijana na anawakilisha maslahi ya vijana na kwamba huu ni wakati wa vijana kuongoza taifa. Ni ujumbe ambao zio rahisi kujua namna vijana watakavyopokea kampeni zao, lakini Bobi wine anaonekana kuvutia sana vijana ambao Museveni anajaribu kuwavutia pia upande wake. Kwa sasa, vijana wapo upande wa Bobi Wine.” Amesema Nabende Wamoto, mchambuzi wa siasa nchini Uganda.

Wamoto anasema kwamba kazi ngumu ni kuhakikisha kwamba vijana hao ambao ni zaidi ya asilimia 76 ya wapiga kura wanajitokeza kushiriki katika zoezi hilo.

Hisia tofauti kuhusu kura za vijana

Dr. Fredrick Golooba Mutebi, mchambuzi wa siasa na uchumi, anadhani kwamba vijana hawatanya maamuzi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2021.

“katika chaguzi zilizopita, vijana wengi walionekana kumuunga mkono Dr. Kiiza Besigye wa FDC kwa sababu walitaka mabadiliko. Ufuasi wao haukuonekana katika hesabu ya kura. Hilo linaweza kujirudia tena.”

Kenneth Lukwago ambaye ni mtangazaji wa muda mrefu anayefanya vipindi vya kisiasa, anasema kwamba kuna pengo kubwa kati ya vijana na maswala ya uongozi. Vijana wengi hawajali zaidi kuhusu mambo ya utawala bora na wanachofanya ni kujaza tu mikutano ya kisiasa na hawajitokezi kupiga kura.

“watu wanapopiga kura mara nyingi wakitafuta mageuzi na mabadiliko lakini hayapatikani, wanachoka kupiga kura na wanakuwa na hisia kwamba hata wakipiga kura, hakuna mabadiliko na hivyo hawajali kupiga kura. Hata wakati tume ya uchaguzi ilipotaka wapiga kura kukagua iwapo wamesajiliwa, hawakufanya hivyo. Yani hawajali”

Kulingana na Lukwago, wapiga kura hawana Imani kwamba uchaguzi unaweza kuleta mabadiliko ya uongozi Uganda

“Idadi kubwa ya watu wanaopiga kura nchini Uganda ni wakaazi wa vijijini na wazee kwa sababu hawana changamoto kubwa sana kama wanazopata watu wanaoishi mijini. Kile wanajali ni usalama wao na wanapoambiwa kwamba usalama umeletwa na Museveni, wanampigia kura. Mengine sio hoja kwao kwa sababu wanapata chakula kutoka kwa mashamba yao” amesema Anderson Lukwago.

Hata hivyo mchambuzi wa siasa Prof David Monda anasema kwamba hadhani kwamba vijana wanaweza kuamua matokeo ya uchaguzi mkuu Uganda.

“Sidhani kama kunaweza kufanyika uchaguzi huru na haki nchini Uganda wakati Museveni amedhibithi kila kitu ikiwemo tume ya uchaguzi na maafisa wa polisi Pamoja na jeshi. Museveni atahakikisha kwamba ameshinda kwa njia zote. Vijana hawatafanya uamuzi wowote katika uchaguzi huu hata wakijitokeza wote kupiga kura.” Amesema Monda akiongezea kwamba demokrasia au mizizi ya demokrasia haijawahi kuota mizizi kwa taifa la Uganda. Tunafanya uchaguzi lakini sio uchaguzi. Ni kumchagua Yoweri Museveni.”

Kulingana na katiba ya Uganda, mshindi katika uchaguzi wa rais lazima apate asilimia 50 au zaidi ya kura zote zilizopigwa, kuepuka duru ya pili.

Rais Yoweri Museveni amekuwa akishinda kwa zaidi ya asilimia 60 japo wapinzani wake wamekuwa wakidai kila mara kuwepo udanganyifu katika hesabu ya kura.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG