Ujumbe wa ngazi ya juu wa serikali ya Marekani umewasili nchini Kenya Jumatatu kutathmini athari za ukame katika ukanda wa Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika na pia kuzungumzia suluhisho la swala hilo na maafisa wa Kenya.
Timu hiyo inayoongozwa na Jill Biden, mke wa Makamu Rais wa Marekani Joe Biden iliwasili Kenya Jumatatu asubuhi. Bi. Biden kisha alienda kwenye kambi ya wakimbizi ya Dadaab ambapo maelfu ya wakimbizi wa Somalia wamekimbilia katika wiki za karibuni kutokana na baa la njaa.
White House inasema safari ya Jill Biden inalenga kuonyesha msaada wa Marekani kusaidia waathirika wa ukame katika eneo la Pembe ya Afrika.
Umoja wa Afrika unasema zaidi ya watu milioni 12 kote katika Pembe ya Afrika wanahitaji msaada wa dharura wa chakula.
Kenya imeepuka baa hilo la njaa linalosambaa kusini mwa Somalia, lakini mashirika ya kutoa msaada ya Umoja wa Mataifa yanasema sehemu kadhaa za nchi hiyo zinahitaji msaada wa dharura wa chakula.
White House inasema Bi. Biden atakutana na Rais wa Kenya Mwai Kibaki na Waziri Mkuu Raila Odinga kuzungumzia njia za kutatua matatizo hayo.
Pia mke huyo wa Makamu Rais wa Marekani, atakutana na waziri wa kilimo wa Kenya kuzungumzia program za chakula za muda mrefu. Jill Biden amefuatana na seneta wa Marekani Bill Frist na Raj Shah, mkurugenzi wa shirika la kimataifa na maendeleo nchini Marekani.