Baraza la kijeshi la Misri limeamuru serikali kufanya uchunguzi juu ya vifo vya watu wasiopungua 25 waliouwawa katika mapigano ya Jumapili mitaani kati ya wakristo wa madhehebu ya Koptik na majeshi ya usalama ya Misri.
Televisheni ya taifa imesema baraza la kijeshi lilitoa amri hiyo Jumatatu baada ya mazungumzo kuhusu mzozo mbaya kuliko wote uliotokea tangu mapinduzi ya February ambayo yalimtoa madarakani rais wa muda mrefu Hosni Mubarak. Majenerali waliochukua madaraka baada ya Bw. Mubarak pia walirudia ahadi yao ya kurudisha madaraka na kuweka utawala wa kiraia.
Baraza la mawaziri la kijeshi la Misri lilifanya mkutano wa dharura Jumatatu. Katika hotuba ya kitaifa iliyotolewa kwenye televisheni jumapili usiku , waziri mkuu Essam Sharraf amesema ghasia zimerudisha nchi hiyo nyuma badala ya kusonga mbele kuelekea kwenye taifa la kisasa lililo chini ya misingi ya kidemokrasia.
Alilaumu mapigano hayo kwa kile alichokiita “mikono iliyofichika” ya wala njama wa nje na ndani lakini hakufafanua.