Jeshi la Nigeria lilisema mji mmoja katika jimbo la Borno ambao umekamatwa na waasi wa kundi la Boko Haram mwezi uliopita umekombolewa tena. Jeshi hilo lilisema kwenye mtandao wake wa Twitter hapo Jumatatu kwamba ‘operesheni ya jeshi ya kusafisha magaidi kutoka Monguno na jamii nyingine ilifanikiwa”.
Jeshi lilisema operesheni ilihusisha mashambulizi ya anga na ilipelekea kukamatwa kwa waasi kadhaa pamoja na malori ya vyakula na bidhaa yaliyokuwa ya wapiganaji wa kundi la Boko Haram katika mji wa Baga.
Hata hivyo jeshi halikusema kama operesheni ilihusisha wanajeshi kutoka Niger, Cameroon au Chad: nchi tatu hizi ambazo kwa hivi sasa zinaisaidia Nigeria kupambana na kundi la waislam wenye msimamo mkali. Kundi la Boko Haram lilifanya mashambulizi katika nchi zote hizo tatu zaidi ya wiki mbili zilizopita.
Jeshi la Nigeria lilisema operesheni ya anga na nchi kavu inaendelea kwa kasi kubwa kuelekea jamii nyingine zilizobuniwa na maeneo yaliyotakiwa kusafishwa.
Monguno, mji wenye kiasi cha watu 100,000 ulitekwa na kundi la Boko Haram hapo Januari 25, huku kundi la haki za binadamu la Amnesty International likikosoa jeshi la Nigeria ikisema lilishindwa kuulinda mji huo licha ya kupata onyo mapema juu ya uwezekano wa kutokea shambulizi lolote la uasi.
Wakati huo huo shirika la habari la Ufaransa linaripoti kwamba idadi ya vifo imeongezeka kufikia 13 kutokana na shambulizi la bomu la kujitoa mhanga siku ya jumapili katika mji wa Damaturu katika jimbo la Yobe. Mashahidi wanasema mwanamke mmoja alijilipua mwenyewe kwenye kituo cha basi kilichojaa watu. Hakuna mtu yeyote aliyedai kuhusika na shambulizi lakini wasi wasi unaelekezwa kwa kundi la Boko Haram ambalo mara kwa mara lilishambulia vituo vya mabasi katika siku zilizopita.
Jumamosi wanamgambo katika mji wa Gombe walisambaza barua wakiwaonya wakazi kutoshiriki kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Upigaji kura awali ulipangwa hapo Februari 14 lakini maafisa wa uchaguzi waliakhirisha uchaguzi huo kwa wiki sita wakisema kundi la Boko Haram kuweka kitisho kikubwa cha usalama nchini humo. Uchaguzi wa urais na wabunge hivi sasa umepangwa kufanyika Machi 28 mwaka huu na maafisa wanasema hautaakhirishwa tena.