Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Juni 03, 2023 Local time: 21:30

Jeshi la Chad limeuchukua tena mji uliodhibitiwa na Boko Haram


Mwanajeshi wa Chad akichungulia kifaru kilichoungua ambacho kinasemekana cha kundi la Boko Haram

Majeshi ya Chad kaskazini mashariki mwa Nigeria katika mji wa Dikwa yanasema yamekamata tena mji huo kutoka kwa wanamgambo wa Boko Haram.

Jeshi liliripoti kwamba wanajeshi 34 walijeruhiwa katika juhudi za kuukomboa mji ambao umekuwa chini ya udhibiti wa Boko Haram kwa wiki kadhaa. Ripoti za ndani zilisema wanajeshi walizunguka mtaa hadi mtaa wakiwatafuta wanamgambo waliobaki ambao bado hawajakimbia.

Jumatatu wanamgambo wa kundi la Boko Haram walitoa mkanda wa video ukionesha kukatwa vichwa kwa wanaume wawili ambao kundi linawashutumu kwa upelelezi.

Video hiyo ya dakika sita iliyotolewa kwenye mtandao inafanana na ile iliyotengenezwa na kundi la wanamgambo wa Islamic State na pia ilikuwa na bendera nyeusi ya IS ikipepea katika eneo la juu upande wa kulia.

Kiongozi wa kundi la Boko Haram
Kiongozi wa kundi la Boko Haram

Hii ni mara ya pili kwa kundi hilo lenye msimamo mkali wa ki-Islam nchini Nigeria kutoa video ikionesha watu kukatwa vichwa. Mara ya kwanza mwezi Oktona mwaka jana ilionesha kundi la Boko Haram likimnyonga mwanamme mmoja anayesemekana kuwa rubani wa ndege iliyopotea ya jeshi la anga la Nigeria.

Video iliyotolewa jumatatu ilipewa kichwa cha habari “Harvest of Spies” inaonesha wanamgambo waliofunika nyuso zao wakiwa na visu virefu wamesimama nyuma ya wanaume wawili waliolazimishwa kupiga magoti ardhini. Kabla ya kumkata kichwa chake, mwanamme mmojawapo aliyejitambulisha mwenyewe kama Dawoud Muhammad wa mji wa Baga ulioko kaskazini-mashariki mwa Nigeria alikuwa anasema amepewa takriban dola 25 kutoka kwa ofisa polisi mmoja kwa ajili ya kufanya upelelezi.

Katika maendeleo mengine hapo Jumatatu jeshi la Nigeria linasema wanamgambo wa Boko Haram walifanya shambulizi jingine katika mji wa kaskazini mashariki wa konduga lakini shambulizi lilizimwa. Maafisa wa jeshi wanasema majibizano ya risasi ya muda wa saa tano siku ya Jumapili yalisababisha vifo vya wanamgambo 72 pamoja na mwanajeshi mmoja. Hakuna uthibitisho huru juu ya idadi ya vifo.

Mwanajeshi aliyeshiriki katika shambulizi aliiambia Sauti ya Amerika-VOA kwamba wanamgambo walijaribu kufanya shambulizi la bomu la kujitoa mhanga kwa gari lililojaa milipuko. Alisema jeshi lilipewa habari kuhusu mpango huo na kwamba mlenga shabaha wa jeshi alimuuwa dereva kabla ya shambulizi kufanyika.

Miji ya Monguno na Konduga, katika jimbo la Borno, Nigeria
Miji ya Monguno na Konduga, katika jimbo la Borno, Nigeria

Mji wa Konduga umekuwa ukishambuliwa mara nyingi katika mwaka uliopita. Kundi la Boko Haram limeuwa maelfu ya watu tangu lianzishe uasi wake mwaka 2009 na kudhibiti miji kadhaa kaskazini-mashariki mwa Nigeria. Nigeria, Chad, Niger na Cameroon walifanya mashambulizi dhidi ya kundi hilo mwishoni mwa mwezi Januari mwaka huu na wameikomboa tena baadhi ya miji.

XS
SM
MD
LG