Jeshi la Pakistan limekanusha ripoti kuwa mmoja wa maafisa wake amekamatwa kwa kusaidia Marekani kumsaka na kumuuwa gaidi Osama Bin Laden na kusema ni uongo usio na msingi wowote.
Msemaji wa jeshi la Pakistan Meja Jenerali Athar Abbas Jumatano alikanusha ripoti hiyo iliyotokea kwanza katika gazeti la New York Times .
Lakini afisa mwingine alikubali kuwa kumekuwa na ukamataji kuhusiana na mashambulizi ya Mei 2 kwenye maficho ya Bin Laden katika mji wa Garrison huko Abottabad.
Msemaji wa jeshi Brigadier Jenerali Syed Azmat Alib aliiambia VOA kwamba hakuna maafisa wa usalama waliokamatwa kuhusiana na uvamizi huo lakini watu wengine kadhaa walikamatwa. Hata hivyo alikataa kuelezea mashitaka dhidi ya hao watu.