Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Desemba 01, 2022 Local time: 08:48

Janga la utekaji nyara watoto laikumba Niger, Nigeria


Rais Muhammadu Buhari

Familia zilizo katika mji wa Kagara kwenye jimbo la Niger katikati ya Nigeria zimekumbwa na majonzi makubwa kutokana na kutekwa nyara watoto wao mapema wiki hii.

Familia hizo zinaitaka serikali kufanya kila liwezekanalo ili kuwapata watoto wao.

Maafisa wa usalama wa Nigeria wanasema wanafuatilia genge lenye silaha linalodhaniwa kuhusika na utekaji nyara, baada ya Rais Muhammadu Buhari kuagiza operesheni ya uokoaji.

Maafisa wa usalama wa Nigeria hapo Alhamis walisema walikuwa wakifuatilia genge lenye silaha lililowateka nyara zaidi ya watu 40 kutoka shuleni siku ya Jumatano, huku familia na manusura wakizungumza na vyombo vya habari kueleza jinsi wanafunzi walivyokimbia waliposikia milio ya bunduki wakati wa shambulizi lililofanyika asubuhi.

Baba wa mwanafunzi mmoja, Mustapha Dauda anasema hajaweza kulala tangu tukio hilo kutokea.

"Siwezi kulala tangu tukio hilo lilipotokea. Serikali tafadhali muokowe kijana wangu. Ataendelea na masomo yake licha ya kitisho dhidi yao, ninaweza kukuhakikishia kwamba atakapo okolewa ataendelea na masomo yake," amesema.

Watu wakihudhuria mazishi ya mwanafunzi aliyeuawa baada ya watu wenye silaha kuvamia shule ya mchipuo wa sayansi ya sekondari ya serikali huko Kagara na kuwateka darzeni ya wanafunzi, jimbo la Niger, Nigeria, Feb. 17, 2021.
Watu wakihudhuria mazishi ya mwanafunzi aliyeuawa baada ya watu wenye silaha kuvamia shule ya mchipuo wa sayansi ya sekondari ya serikali huko Kagara na kuwateka darzeni ya wanafunzi, jimbo la Niger, Nigeria, Feb. 17, 2021.

Utekaji nyara huko Kagara, katikati ya jimbo la Niger utekaji mwingine mkubwa wa hivi karibuni nchini Nigeria, mahala ambapo magenge ya wahalifu yanayo julikana kama majambazi yameongeza mashambulizi dhidi ya vijiji na miji.

Kulingana na maafisa wa jimbo la Niger, watu wenye silaha waliovalia sare za jeshi walivamia na kushambulia chuo cha sayansi cha serikali, “Government Science College huko Kagara mapema Jumatano, na kumuuwa mwanafunzi mmoja na kuwatelekeza wengine kwenye msitu ulio karibu.

Watekaji nyara waliwachukua watu 42 wakiwemo wanafunzi 27, waalimu watatu na ndugu wengine wa wafanyakazi wa shule.

Caleb Samaila mwenye miaka 18, ni mmoja kati ya wanafunzi waliobahatika kukimbia wakati wa shambulizi hilo la asubuhi.

Caleb Samaila, mwanafunzi anaeleza : "Siku hiyo nilikua nimelala bwenini, kisha nilisikia watekaji nyara wanakuja kwenye mabweni yetu na walianza kufyatua bunduki. Nilitoka nje na niliwaona kisha nikakimbia na kuruka juu ya senyeng’e. Kulikuwa na wanafunzi wengine pia ambao walikuwa wakikimbia kupitia njia mbali mbali."

Haikufahamika mara moja nani alihusika na utekaji huu wa mwisho. Utekaji nyara kwa ajili ya kudai fidia unaofanywa na vikundi vyenye silaha ni jambo la kawaida katika majimbo mengi ya kaskazini mwa Nigeria.

Shambulio hilo lilitokea miezi miwili baada ya watu wenye silaha kuvamia shule ya upili katika jimbo la kaskazini magharibi la Katsina na kuwateka nyara wavulana takribani 350 ambao baadae waliokolewa na wanajeshi wa usalama.

Kundi la kutetea haki za za binadamu la Amnesty International limesema katika taarifa yake kwamba elimu inashambuliwa kaskazini mwa Nigeria.

Mfanyabiashara Ahmed Yakubu anasema hali ni mbaya katika jimbo hilo.

Yakubu anasema : "Kwa kweli hali ya usalama ni mbaya sana hata sijui itatokea vipi kwa sababu sioni haja ya watu kuja na pikipiki kwa idadi isiyozidi 23,30 au 50 sio zaidi ya hapo na wataingia kwenye kijiji watafanya operesheni kwa mafanikio, wataondoka bila ya kukabiliwa hata kidogo."

Rais Muhammadu Buhari alituma wakuu wa usalama kuratibu shughuli za uokoaji, msemaji wake Garba Shehu alisema katika taarifa.

Jeshi la Nigeria lilisema katika taarifa kwamba limekusanya wanajeshi ambao wanawafuata watekaji nyara na mkuu wa polisi wa nchi hiyo alisema maafisa wake wanashirikiana na idara ya usalama ya serikali kuu ili kuimarisha usalama katika jimbo ambalo utekaji nyara ulifanyika.

Mashambulizi ya karibuni yameibua wasiwasi juu ya kuongezeka kwa vurugu na magenge yenye silaha na waasi wa kiislam. Na kusababisha Buhari kukosolewa kwa jinsi anavyoshughulikia usalama wa taifa.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG