Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton amesema kukamatwa kwa rais wa zamani wa Ivory Coast Laurent Gbagbo kunaonesha kwamba kuwepo kwa madiktekta na viongozi wakaidi watawajibishwa kama watajaribu kung’ang’ania madaraka.
Akizungumza mjini Washington jumatatu waziri Clinton amesema hatua hiyo inatuma ishara kuwa viongozi wasidharau sauti za watu wao katika uchaguzi ulio huru na haki.
Clinton amesihi raia wa Ivory Coast kuwa watulivu na marekani inatarajia kufanya kazi na rais mteule Alassane Ouattara kupanga maridhiano.
Maafisa wa ufaransa wanasema rais Nicolas Sarkozy alikuwa na mazungumzo ya muda mrefu na bwana Ouattara kwa njia ya simu baada ya mzozo kufikia mwisho.
Mkuu wa maswala ya usalama wa umoja wa mataifa Alain Le Roy amesema jambo muhimu hivi sasa ni kujaribu kurejesha usalama , kuanza taratibu za maridhiano na kushughulikia mzozo mkubwa wa kibinaadamu uliosababishwa na ghasia za Ivory Coast.
Ivory Coast: Marekani kufanya kazi na Ouattara

Waziri wa mambo ya nje Hillary Clinton asema Marekani iko tayari kufanya kazi na Rais mteule wa Ivory Coast Allasane Ouattara