Wanajeshi wa Israel wameanzisha mashambulizi mapya leo Ijumaa katika mji wa Khan Younis kusini mwa Gaza, wakiwalenga wapiganaji wa Hamas ambao jeshi linadai bado wanafanya operesheni zao huko licha ya mashambulizi ya mara kwa mara, wakati wapatanishi wa Marekani, Qatar na Misri wakianzisha tena shinikizo lao kwa Israel na Hamas kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano.
Amri za Israel za kuhama kwa Wapalestina zilisababisha wimbi jingine la Wapalestina kutoka wilaya za mashariki za Khan Younis zilizoharibiwa sana, ambako wengi walikuwa ndiyo kwanza wamerejea chini ya wiki mbili zilizopita, baada ya uvamizi wa mwisho wa jeshi la Israel mjini humo mwezi Julai.
Maelfu walikimbia Alhamisi, wakiwa wamebeba vitu muhimu kama vile mitungi midogo ya gesi, magodoro, mahema, mifuko ya kuvaa mgongoni na mablanketi. Maafisa kutoka Israel na Marekani wamesema wanaamini Yahya Sinwar, kiongozi mpya aliyetajwa wa Hamas na mmoja wa wapangaji wa shambulio la Oktoba 7 dhidi ya Israel, anaweza kujificha katika mahandaki chini ya Khan Younis.
Forum