Mkuu wa shirika la Fedha la kimataifa (IMF), Christine Lagarde amesema leo Ijumaa kuwa wazo la Uingereza kujiondoa kutoka kwenye Umoja wa Ulaya (EU) lina uwezekano wa kulitumbukiza taifa hilo kwenye hali ya kudorora kwa uchumi wake.
Mapema mwaka huu IMF ilionya kuwa hatua hiyo ingepelekea kushuka kwa thamni ya nyumba na hisa iwapo wapiga kura wa Uingereza wataamua kujiondoa katika umoja huo kupitia kura ya maoni ya Juni 23.
Viongozi wa zamani wa NATO kwenye barua ya awali kwa gazeti la Daily Telegraph la Uingereza walikuwa wamesema kuwa kujiondoa kwa Uingereza kwenye umoja huo kungewapa maadui nafasi wakati ulaya inapohitajika kuungana.
Rais wa Marekani, Barack Obama kwenye taarifa ya pamoja akiwa na waziri mkuu wa Uingereza, David Cameron mjini London mwezi uliopita alisema kuwa kubaki kwenye umoja huo kunaipatia Uingereza ushawishi mkubwa. David Cameron kwa upande wake ameonya dhidi ya kujiondoa kwenye umoja huo akitoa sababu za kiusalama na kiuchumi.