Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 19, 2024 Local time: 09:18

IEBC yawasilisha maelfu ya stakabadhi mahakamani Kenya


Maafisa wa IEBC wakihesabu fomu katika ukumbi wa Bomas of Kenya.
Maafisa wa IEBC wakihesabu fomu katika ukumbi wa Bomas of Kenya.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini Kenya, IEBC, Jumanne iliwasilisha kurasa 54,000 za stakabadhi kwenye mahakama ya juu.

Hii ni baada ya muungano wa NASA kuwasilisha ushahidi wenye kurasa 25,000 katika Mahakama hiyo kupinga ushindi wa Rais Kenyatta. Nyaraka hizo ni majibu ya masuala yaliyoibuliwa na muungano huo.

Stakabadhi hizo zinajumuisha fomu namba 34 a, b na c pamoja na karatasi nyingine zitakazotumiwa na mawakili wake kujibu madai yaliyoibuliwa na NASA katika kupinga ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta.

Kulingana na utaratibu wa mahakama, IEBC ilistahili kuwasilisha stakabadhi hizo siku mbili baada ya uchaguzi.

Kwa mujibu wa wataalamu wa sheria za uchaguzi nchini Kenya, baada ya IEBC kuwasilisha stakabadhi zake, rais Uhuru Kenyatta ana hadi Alhamisi jioni kuwasilisha majibu yake kabla ya kujibu hoja zitakazowasilishwa na NASA kufikia Ijumaa.

"Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Jaji Mkuu David Maraga, hoja za walalamikaji zitajibiwa kufikia saa moja jioni Ijumaa huku walalamikaji wakiruhusiwa kujibu hoja za washtakiwa kufikia Jumamosi," mchambuzi mmoja aliieleza Sauti ya Amerika kutoka Nairobi.

Baadaye Jumapili, mahakama inatarajiwa kufanya kikao cha mwanzo kuamua jinsi ya kuishughulikia kesi hiyo kabla ya vikao vya mahakamani kuanza. Uamuzi unatarajiwa Ijumaa wiki ijayo.

Huku hayo yakiarifiwa, aliyegombea urais kwa tiketi ya NASA, Jumanne alisisitiza haja ya Mahakama ya Juu kutenda haki.

Raila Odinga aliizungumza wakati wa kuapishwa kwa Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho, ambapo alitilia mkazo kauli kwamba mbali na uchaguzi wa urais, magavana kadhaa wa Jubilee vilevile walichaguliwa kwa njia ya udanganyifu.

"Ni lazima tabia ya kuiba kura iishe nchini Kenya. Hatutasahau na kuendelea na maisha," alisema Odinga.

XS
SM
MD
LG