Wanasiasa wamekuwa wakidai kwamba uamuzi wa IEBC ulikuwa wa kisiasa kuwafanya wapiga kura kutojitokeza kwa wingi kuwapigia kura.
Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati amesema kwamba uchaguzi wa ugavana katika kaunti za Mombasa na Kakamega, pamoja na uchaguzi wa wabunge katika maeneo ya Kacheliba na Pokot Kusini uliahirishwa kutokana na makosa wakati wa uchapishaji wa karatasi za wapiga kura.
“Hatufanyi siasa, tunasimamia uchaguzi. Waliochapisha karatasi wamekubali kwamba walifanya makosa na wameomba msamaha,” amesema Chebukati.
Tume ya uchaguzi imesema kwamba picha za wagombea hazikulingana na majina.
“Kwa sababu hiyo, uchaguzi wa wagombea hao hautafanyika. Tarehe mpya itatangazwa kupitia gazeti rasmi la serikali.” Chebukati amewaambia waandishi wa habari katika ukumbi wa Bomas, Nairobi Kenya.
Kampuni ya Lykos, ya Ugiriki, ndiyo iliyopewa zabuni ya kuchapisha karatasi za kura.