Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Julai 15, 2024 Local time: 05:03

Chebukati ni mwenyekiti mpya wa IEBC Kenya


Bunge la Kenya
Bunge la Kenya

Bunge la taifa la Kenya limempitisha Wanyonyi Chebukati kuwa mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (IEBC) nchini Kenya.

Takriban wiki mbili zimepita tangu rais Uhuru Kenyatta alipomteua wakili Chebukati katika nafasi hiyo baada ya Isaak Hassan kuondolewa kufuatia shinikizo la vyama vya upinzani.

Bwana Chebukati pamoja na makamishna sita wameidhinishwa na bunge la taifa kuiongoza tume hiyo wakati Kenya inajitayarisha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu miezi michache ijayo.

Makamishna sita ambao uteuzi wao umeidhinishwa pia na bunge ni Consolata Nkatha Bucha, Dkt Roselyn K. Akombe, Margaret Wanjala Mwachanya, Boya Molu, Profesa Abdi Guliye na Balozi Paul Kurgat.

Wakati akihojiwa na kamati ya bunge ya Haki na Sheria, Chebukati alilaumiwa kwa kuonyesha udhaifu katika masuala ya kisheria, madai ambayo aliyakanusha.

Vile vile Chebukati alitakiwa kuelezea waziwazi uhusiano wake na kiongozi wa upinzani Bw Raila Odinga baada ya kuripotiwa kuwa alikuwa anawania ubunge katika chama anachokiongoza Bw Odinga.

Chebukati alisisitiza kuwa alikuwa mwanachama wa chama hicho lakini alijiuzulu mwezi mmoja kabla ya kutuma maombi ya uenyekiti wa IEBC.

Hata hivyo kamati ya Haki na Sheria ikiongozwa na mwenyekiti wake ambaye pia ni mbunge wa Ainabkoi, Samuel Chepkonga ameeleza kulikuwa hakuna malalamiko yoyote yaliyofikishwa mbele yake kupinga uteuzi wa Bw Chebukati.

Zoezi la kuwaajiri makamishna wapya linafuatia kupitishwa kwa sheria kuhusu IEBC baada ya kuwepo makubaliano ya kisiasa kati ya vyama vikuu vya kisiasa nchini; Jubilee na CORD baada ya maandamano yaliyoitishwa na wapinzani yakishinikiza kuondolewa madarakani Isaak Hassan aliyekuwa mwenyekiti wa tume hiyo.

Chebukati na makamishna hao sita sasa wanatarajiwa kuapishwa na rais Kenyatta kuanza mara moja zoezi la usajili wa wapigaji kura

Imetayarishwa na mwandishi wetu Kennedy Wandera,Nairobi, Kenya

XS
SM
MD
LG