Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Aprili 28, 2024 Local time: 22:47

Idadi kubwa ya Watanzania waunga mkono maadamano Dar es Salam


Baadhi wa watu walioshiriki katika maandamano jijini Dar Es Salaam. Picha na VOA
Baadhi wa watu walioshiriki katika maandamano jijini Dar Es Salaam. Picha na VOA

Idadi kubwa ya Watanzania wamejitokeza na kuunga mkono maandamano ya amani yaliyoandaliwa na chama kikuu cha upinzani Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) yaliyofanyika Jumatano.

Maandamano hayo yaliyoanzia jijini Dar-es Salaam, na kuendelea katika miji mingine yanapinga kupanda kwa gharama za maisha na kudai kusikilizwa kwa maoni ya wananchi na wadau wa demokrasia katika masuala ya sheria ya uchaguzi.

Waongozi wa maandamano hayo walifikisha ujumbe wao katika ofisi za Umoja wa Mataifa, unaoitaka serikali ya Tanzania kushughulikia changamoto za kupanda kwa gharama za maisha zinazowakabili wananchi pamoja na mageuzi ya katiba.

Mratibu wa mtandao wa vuguvugu la katiba, Buberwa Kaiza amesema sababu ya maandamano hayo kuishia katika ofisi za Umoja wa Mataifa ni kutoa ujumbe duniani kupitia umoja huo kuwa miswaada ya sheria ya uchaguzi iondolewe bungeni.

“Sababu kubwa ya kuja hapa Umoja wa Mataifa ni kutoa ujumbe duniani kote kupitia umoja huu kwamba madai haya ya sheria hizi ziondolewe bungeni yapate nguvu yaweze kusikilizwa kwa namna ambavyo inatarajiwa.” Kaiza

Waandamanaji wakiwa na mabango yao
Waandamanaji wakiwa na mabango yao

Maandamano hayo yanafanyika kufuatia muswaada wa sheria ya uchaguzi kushindwa kutatua changamoto zilizopo ikiwemo uchaguzi wa serikali za mitaa kusimamiwa na TAMISEMI, kupanda kwa gharama za maisha kutokana na baadhi ya bei za bidhaa kupanda ikiwemo sukari na vyakula pamoja na kukosekana kwa kipindi kirefu cha umeme wa uhakika.

Mchungaji Peter Msigwa ni miongoni mwa wanasiasa walioshiriki maandamano hayo, alisema sababu zingine za maadamano hayo ni ukosefu wa ajira kwa vijana, kutoridhishwa kwa usimamizi wa miradi mikubwa ya maendeleo pamoja na ongezeko la deni la taifa.

“Tunatuma ujumbe hatutaki taifa ambalo umeme unakatika bila sababu, hatutaki taifa ambalo hakuna ajira, miradi yote mikubwa ya maendeleo imekufa sasahivi haiendelei taifa ambalo sasahivi SGR imesimama,” aliesma Msigwa.

Na kuongeza kuwa “deni la taifa limefika karibuni trilioni mia moja sasa tutafika wapi, maandamano haya ni kupeleka taarifa kwa watawala wasipotusikia kwa midomo watatusikia kwa miguu na huu ni mwanzo tu.”

Waandamanaji huko Dar Es Salaam
Waandamanaji huko Dar Es Salaam

Naye Dkt Ananilea Nkya miongoni mwa wanaharakati na wananchi walioshiriki katika maandamano hayo ameitaka serikali kusikiliza vilio vya wananchi na kufanya kila njia ili kupunguza gharama za maisha pia amewataka wananchi kujitokeza na kutetea maslahi yao kupitia maandamano hayo.

Alisema “Lazima tusimame tutoe sauti ili nchi yetu tuweze kupata maisha bora kuliko yalivyo hivi sasa kwahiyo tafsiri ya haya yote ni kwamba lazima serikali isikie maoni ya wananchi katika mambo yafuatayo la kwanza kwamba tunahitaji katiba mpya”

Akizungumza baada ya kutoka katika ofisi za Umoja wa Mataifa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Freeman Mbowe alisema baada ya kuwasilisha ujumbe wao katika ofisi za Umoja wa Mataifa nchini Tanzania wanasubiria ujumbe huo kufikishwa kwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Forum

XS
SM
MD
LG