Karim Khan, amesema ameomba idhini ya kuanza kusikilizwa rasmi kwa kesi dhidi ya kiongozi huyo wa kundi la Lords resistance movement LRA, ambaye ni mshukiwa wa muda mrefu zaidi katika mahakama hiyo ya ICC na ambaye hajakamatwa.
Khan alisema hii ni mara ya kwanza kwa ofisi yake kutoa ombi kama hilo tangu mahakama ya ICC ilipoanzishwa na kusisitiza kwamba ni muhimu na sahihi kabisa kwa kuanzisha mashtaka dhidi ya Kony na kesi kusikilizwa hadi mwisho.
Hati ya kukamatwa kwa Kony, mwanzilishi wa kundi la waasi la LRA, ilitolewa mwaka 2005.
Anakabiliwa na mashtaka 33 ya uhalifu wa vita na uhalifu dhidi ya binadamu, yanayohusisha mauaji, kuteka watu nyara, ubakaji na kushambulia raia.
Kundi la LRA, likiongozwa na Kony, lilishambulia raia wa kaskazini mwa Uganda kwa karibu miaka 20 huku likipigana na serikali ya Rais Yoweri Museveni.
Inaaminika kwamba kundi la LRA halina nguvu tena, na Joseph Kony amekwepa mtego wa kukamatwa kwa zaidi ya miaka 17.
Mnamo mwezi May 2021, ICC ilimhukumu Dominic Ongwen, mmoja wa wailiokuwa makamanda wa LRA, aliyejiunga na kundi hilo akiwa mtoto, miaka 25 gerezani kwa makosa ya ubakaji, dhuluma za kingono, kuteka nyara Watoto, mateso na mauaji.