Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Machi 19, 2024 Local time: 08:13

Hotuba ya mwisho: Obama asema Marekani ‘itakuwa sawa’


Rais Barack Obama akiwashukuru waandishi wa habari katika Ikulu ya White House, Washington.
Rais Barack Obama akiwashukuru waandishi wa habari katika Ikulu ya White House, Washington.

Katika mkutano wa mwisho na waadishi wa habari Jumatano Rais Barack Obama alichukua fursa hiyo kuwahakikishia wamarekani nchi itaendelea kuwa salama.

Hilo linatokana na kuwepo wale wenye wasiwasi kuhusu mabadiliko ya kiutawala yaliyotokea baada ya miaka minane ya kuwa yeye ni kiongozi: “Nina imani na nchi hii. Nina imani na watu wa Marekani. Nina imani kuwa watu wengi ni wema kuliko watu waovu.”

Waandishi wa habari wanaoripoti kutoka Ikulu ya White House walimuuliza Obama kuhusu hatua yake yenye utata ya kufupisha kifungo cha aliyekuwa mchambuzi wa kipelelezi jeshini, Chelsea Manning, na mambo mengine. Rais aliyajibu hayo kwa urahisi, lakini alichukua muda kuelezea suala la mwisho aliloulizwa, vipi yalikuwa mazungumzo yake na watoto wake Malia na Sasha kuhusu matokeo ya uchaguzi wa Marekani.

Obama amesema kuwa Malia na Sasha walikuwa wameshtushwa na ushindi wa mgombea wa Republikan dhidi ya chaguo lake mgombea wa Demokratik Hillary Clinton, kama walivyo shangazwa yeye na mkewe, Michelle, lakini anaona fahari juu yao kwa ushupavu wao, utaifa na sio wenye kukata tamaa.

Obama akubali anaghadhibika

Rais alikubali taswira yake kwa umma --ni ya utulivu na uchangamfu- sio kuwa ndio uhalisia wake vile anavyokuwa wakati akiwa amejifungia peke yake.

“Ninakuwa tofauti zaidi kuliko ninapokuwa katika hadhara, na wakati mwengine nakuwa nimechanganyikiwa na nimeghadhibika, kama vile kila mtu mwengine anavyokuwa,” alisema. “Lakini kimsingi nafikiri tutakuwa vizuri (kama nchi). Lazima tulipiganie hilo, lazima tujishughulishe kufikia hilo na tusichukulie kirahisi, na najua nyinyi mtatusaidia kufikia hilo.”

Amesema watoto wake wanaelewa hilo “ kitu pekee ni kwamba mwisho wa dunia ni mwisho wa dunia.”

Obama amewashukuru wanachama wa jumuiya ya waandishi wa ikulu ya White House, akawapungia mkono na kugeuka na kuondoka katika chumba cha Brady cha habari, ambacho kilikuwa kimefurika waandishi. Akitoa kauli ya upole na mara nyingine ya huzuni, alisema kuwepo kwa waandishi White House ilimfanya kuwa rais bora zaidi na uhuru wa habari ni muhimu kwa demokrasia.

Awafunda waandishi wa Habari

Kwa nyinyi waandishi, amesema: “Hamtakiwi kuwa mnao kubali kila kitu. Mnatakiwa kuwa na mashaka na kila kitu. Mnatakiwa kuuliza maswali magumu.”

Hilo lilikuwa limetokana na mjadala mkubwa ulioko kati ya jamii ya wanahabari kuwa kuna uvumi kwamba wasaidizi wa Donald Trump wana mpango wa kulihamisha kundi la waandishi wa habari wa White House kutoka katika chumba wanachokutania karibu na ofisi ya rais ya Oval, kwenda eneo mbali na hapo pengine katika jengo jingine.

Kufuta mashtaka

Suala la kwanza aliloulizwa Obama Jumatano ni juu ya kufuta kifungo cha miaka 35 alichohukumiwa Manning

Chelsea Manning
Chelsea Manning

kwa kuvujisha nyaraka za siri za kijeshi.

Ilivyokuwa Manning tayari ameshatumikia kifungo kirefu zaidi kuliko wale waliokuwa wamehukumiwa kwa kosa kama hilo, na kuwa amekubali kuwa alipaswa kuwajibika kwa matendo yake, Obama amesema:” Kwa mtizamo wa mazingira hayo yote, kufuta adhabu hiyo ilikuwa ni sawa kabisa.”

Obama amesema hakuona tofauti yeyote katika kutoa msamaha wa rais kwa Manning wakati amekuwa mstari wa mbele kulaani kitendo cha udukuzi wa Russia katika hujuma ya mitandao kwenye kampeni za urais za Marekani, ikihusisha madai ya wizi wa barua pepe zilizo wadhalilisha maafisa wa chama cha Demokratik.

“Pia alitupilia mbali ahadi ya kikundi cha Wikileaks kinachopinga udhibiti wa siri kilichoundwa na Julian Assange, kuwa atakubali kushtakiwa Marekani iwapo Manning ataachiliwa: “ Siupi uzito mkubwa ujumbe anaotuma Bw Assange katika Tweeter, kwa hilo halikuwa katika fikra yangu.”

Obama amesema amejaribu kuwashawishi Russia wapunguze mlundikano wa silaha za nyuklia, lakini kiongozi huyo wa Kremlin, Vladimir Putin amekuwa mkaidi kuzungumzia hilo, na ana matumaini kuwa mrithi wake ataweza kuendeleza mazungumzo kuhusu suala hilo la kupunguza silaha za nyuklia

Azungumzia ubabe wa Russia

Akigeukia katika suala zito zaidi la jukumu la Marekani katika medani ya ulimwengu, rais amesema vikwazo vilivyowekwa kwa Russia baada ya kuvamia mkoa wa Crimea ulio sehemu ya Ukraine ni “mfano mzuri wa jukumu kubwa” linalofanywa na Marekani. Pia amehimiza utawala unaoingia madarakani kuendeleza kuzizuia nchi kubwa “kuzikandamiza” nchi ndogo.

Kwa ujumla, Obama amesema kukabidhiana madaraka kati yake na timu ya Trump kunaendelea “vizuri.”

Obama aligusia kuwa Trump alishinda uchaguzi wa urais kwa kupinga juhudi nyingi alizozisimamia katika miaka yake minane. Rais mpya ataendelea na dira yake na itikadi zake, Obama amesema, na “ Sitarajii kuwa kutakuwa na muingiliano mkubwa” kati ya sera na malengo ya uongozi wa pande hizi mbili.

Obama amesema atazungumza tu kumkosoa Trump iwapo anahisi kuwa maadili ya msingi ya Marekani yako hatarini, ikiwa litahusisha kuzuia haki ya kupiga kura, sera kali dhidi ya uhamiaji au kuwashambulia waandishi wa habari.

Hata hivyo alikataa kuongea kuhuse suala la mgomo unaandaliwa kususia kuapishwa kwa Trump siku ya Ijumaa ambapo wabunge zaidi ya 50 wamekubaliana kufanya hivyo. Rais Obama anayemaliza ngwe yake na mkewe watahudhuria sherehe hizo hapo kwenye bunge la Marekani kushuhudia kuapishwa kwa rais.

Ujumbe kwa Taifa

Katika ujumbe wake wa taifa moja bila ya ubaguzi, Obama amesema kwamba anategemea siku za usoni kuona mwanamke, mlatino, myahudi, Mhindu wote wanakuwa marais na wengi wengineo hapa Marekani.

Obama amewakumbusha waandishi kuwa kuna kazi kubwa katika kukabiliana na “habari za uongo” kama yale madai ya mwaka jana – yote hayo yamethibitishwa ni uongo- kwamba uchaguzi waMarekani utayumbishwa kwa sababu ya wizi wa kura. Rais amesema kuna “historia ya kushusha” nyuma ya kadhia yote ya kuzuilia watu wasipige kura Marekani ikiwa na mizizi yake tokea zama za utumwa.

Suala jingine lenye utata ni lile la uamuzi wa Obama kusitisha kilichokuwa kinajulikana kama sera ya wahamiaji wa Cuba “wet foot, dry foot” kwa sababu haina mashiko hivi sasa, kwa kuwa kumekuwa na mafungamano yanayoendelea kati ya Marekani na Cuba.

Dhana ya sera hiyo ya “wet foot, dry foot” ilikuwa ni ile hali ya mhamiaji wa Cuba akikamatwa baada ya kuingia Marekani anaruhusiwa kuishi kama mhamiaji na kama akikamatwa baharini anarudishwa Cuba.

Kuhusu mashariki ya Kati, Rais amesema kuwa “inawezekana fursa hiyo imepotea” kwa kuweza kuwa na mataifa mawili kama suluhisho la mgogoro wa Israeli na Palestina, lakini akasema anavyohisi yeye matabaka haya hayawezi kuendelea Israeli.

XS
SM
MD
LG